Ukata Jumuiya ya Afrika Mashariki unavyoumiza wafanyakazi wake

Arusha. Migogoro ya kifedha ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki imezidi kuitafuna taasisi hiyo kubwa baada ya kusitisha ghafla ajira za watumishi 47 wa muda.

Watumishi hao waliokuwa na mikataba ya muda, walishindwa kuongezewa baada ya baraza la mawaziri kushindwa kukubaliana juu ya kutoa ruhusa za kuongezewa mikataba.

Kati ya watumishi 47 waliopoteza ajira zao 22 ni watanzania, 18 ni kutoka Uganda, wengine nne ni Kenya na wawili kutoka Rwanda na wengine Burundi.

Kutokana na hilo, wafanyakazi hao wamejitokeza hadharani kuwaomba wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuingilia kati suala lao ili waweze kuongezewa muda wa kufanya kazi ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Hatuna la kufanya zaidi tunaomba wakuu wa nchi waingilie kati sakata hili tuongezewe mikataba tena kwani tumetumikia jumuiya hii kwa zaidi ya miaka 10 na wengine miaka 18 tukisaini mikataba ya miezi sita au mwaka kwa ahadi kuwa bado ajira za muda mrefu hazijatoka,” amesema mmoja wa wafanyakazi hao ambao hawakutaka kutajwa majina.

Akielezea sakata hilo lilivyokuwa, Mfanyakazi Daniel (sio jina lake halisi) amesema kuwa ameanza kazi katika Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki tangu mwaka 2009 kitengo cha fedha na kupewa mkataba wa mwaka mmoja.

“Niliendelea kufanya kazi na kila mara mkataba ukiisha tunaongezewa muda wa mwaka mmoja tena hadi leo hii,” amesema na kuongeza;

“Mwaka jana tuliuliza kuhusu hatma yetu lakini tuliambiwa tuendelee na kazi na endapo ajira za moja kwa moja zikitangazwa tutaomba na tutapewa kipaumbele kama watumishi tuliojitoa na kufanya kazi kwa muda mrefu ndani ya jumuiya bila baadhi ya stahiki kutokana na sio wafanyakazi kamili,” amesema.

Amesema kuwa mikataba mingi huisha mwezi Juni na walipotarajia kuongezewa waliambiwa waendelee na kazi kusubiri hatima yao baada ya vikao vya baraza la mawaziri wa EAC ambao ndio huamua ajira za wafanyakazi.

“Tulifanya kazi bila mikataba kwa matumaini makubwa hadi mwezi Septemba ambapo baraza la mawaziri liliitishwa kwa ajili ya kuamua hatima yetu, lakini badala yake tulisikia kikao kimevurugika bila kufikia muafaka,” amesema.

Amesema kuwa baada ya kikao kile kuvunjika kesho yake walipokea barua kutoka kwa mkurugenzi rasilimali watu kutakiwa kukabidhi kila kitu na kuacha kazi.

“Tulishangaa sana na kuuliza kulikoni bila majibu na hadi leo tuko njia panda hatuelewi nini cha kufanya,” amesema “Tunaomba msaada maana wengine tuna familia hapa zinatutegemea lakini wangetupa muda wa kujipanga ingekuwa bora maana tumetumikia jumuiya kwa muda mrefu wasitulipe maumivu ya namna hii.”

Awali katika kikao cha 35 cha baraza la mawaziri wa EAC waliokutana ndani ya makao makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yaliyoko jijini Arusha Septemba 9, 2025 pamoja na mambo mengine walikuwa na jukumu la kujadili na kupitisha maombi ya wafanyakazi wa muda kuongezewa mikataba.

Katika baraza hilo ambalo Kenya kwa sasa ndio mwenyekiti kilishindwa kufikia muafaka katika kipengele cha ajira za watumishi wa muda baada ya wajumbe kutoka Kenya kutoka nje na kususia ajenda hiyo.

Uongozi huo ulidai kuwa hawawezi kuendelea kuongeza mikataba ya wafanyakazi wa muda wakati fedha za kulipa mishahara yao hakuna kutokana na nchi wanachama kushindwa kulipa michango yao wanayopaswa kulipa.

Aidha EAC yenye wanachama nane kila nchi inapaswa kulipa mchango wa dola milioni 7 kila moja (sawa na jumla ya dola milioni 56) kabla ya mwisho wa Juni 2025.

Hadi mwezi Juni mwaka huu, ripoti inaonyesha nchi zilizokamilisha michango yao ni nchi waanzilishi wa jumuiya hii ambao ni Uganda (102%) Tanzania (100%) na Kenya (100%).

Wengine waliochangia ni Rwanda (75), Somalia (50), Burundi (19%), DRC (14) huku Sudani Kusini akichangia asilimia saba pekee.

Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Ardhi Kame na Ukame na Maendeleo ya Kikanda wa Kenya, Beatrice Askul Moe, ambaye ndiye mwenyekiti wa baraza alisema ajira mpya zitaamuliwa kulingana na maamuzi ya baraza.

“Hatukatai kuajiri watumishi ambao wametumikia taasisi hii kwa muda mrefu lakini tunapata wapi fedha za kuwalipa mishahara wakati baadhi wanachama hawataki kutimiza wajibu wao wa kulipa michango? Tusubiri wakuu wananchi wanasemaje kuhusu michango ndio suala la ajira mpya zitaamuliwa,” alisema.

Katibu Mkuu wa EAC, Veronica Nduva alisema kuwa anasubiri busara za baraza hilo lakini pia wakuu wa nchi ili aitishe tena kikao cha ajenda hiyo.

“Uzuri niliwaandikia barua nchi zote na sita wakakubali ziongezwe lakini mwenyekiti akaomba tukutane kujadili hili ana kwa ana na tulipokutana ndipo muafaka ukashindikana hivyo tupeni muda tuitishe kikao kingine tujadili tena na maamuzi mazuri tuna imani yatapatikana,” amesema.

Kwa mujibu wa taarifa ya Baraza la Mawaziri jumuiya hiyo ina jumla ya nafasi 420 za ajira katika taasisi zake zote huku nafasi 152 bado hazijajazwa, na wafanyakazi wengine 33 wanatarajiwa kuondoka hadi Desemba 2025 kutokana na mikataba kumalizika au kustaafu.