USHIRIKIANO WA AFRIKA NA NORDIC NI NGUZO YA AMANI NA MAENDELEO ENDELEVU

:::::

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, amesisitiza umuhimu wa Mkutano wa nchi za Afrika na nchi za Nordic kama jukwaa muhimu la kujadili changamoto zinazokabili Bara la Afrika na kupata suluhu za pamoja kupitia ushirikiano wa kimataifa.

Akizungumza katika Mkutano wa 22 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje kati ya nchi za Afrika na nchi tano za Nordic (Denmark, Norway, Sweden, Iceland na Finland), Waziri Kombo alibainisha kuwa migogoro mingi duniani, ikiwemo barani Afrika, imekuwa ikichochewa na masuala ya mipaka, rasilimali, ukosefu wa ajira kwa vijana, tofauti za kikabila na udhaifu wa mifumo ya kuzuia migogoro kabla hazijazuka.

Alisisitiza kuwa majukwaa ya kimataifa yana nafasi kubwa ya kusaidia kutatua changamoto hizo kwa kuunganisha nguvu na maarifa ya pamoja. Aidha, alibainisha kuwa msingi wa kudumu wa usalama barani Afrika ni kinga na kuzuia migogoro, badala ya kusubiri izuke. Waziri Kombo pia alieleza kuwa teknolojia na ubunifu ni nyenzo muhimu za kuendeleza jamii na kujenga mustakabali wa amani na maendeleo endelevu.

Waziri Kombo pia amesisitiza umuhimu wa kushughulikia changamoto ya ajira kwa vijana barani Afrika kwa kuwa vijana ni rasilimali kubwa ya maendeleo ya bara. Amesema ni lazima kuwekeza katika sera na programu za kuongeza ajira, kukuza stadi za ubunifu na kuimarisha matumizi ya teknolojia ili vijana washiriki kikamilifu katika kujenga uchumi imara na jamii yenye amani endelevu.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara za Kimataifa wa Zimbabwe, Prof. Amon Murwira, akifunga mkutano huo, alisema majadiliano yameangazia ushirikiano wa pamoja katika sayansi, teknolojia na ubunifu, huku kipaumbele kikiwa ni kuongeza sauti za vijana katika maamuzi ya sera na kuimarisha mifumo ya ubunifu inayoendeshwa na vijana.

Prof. Murwira alitaja sekta za kimkakati zilizopatiwa kipaumbele kuwa ni nishati safi, ajira, miundombinu, kilimo kinachokabiliana na mabadiliko ya tabianchi na uchimbaji endelevu wa madini. Alisisitiza kuwa lengo kuu la mkutano ni kuoanisha sera, kuhamasisha uwekezaji wa pamoja na kubadilisha mifumo ya ushirikiano kutoka utegemezi wa misaada ya nje kwenda kwenye msingi wa biashara na uwekezaji. Pia alieleza umuhimu wa kuimarisha miundombinu ya reli na kuanzisha jukwaa la uratibu ili kuhakikisha maazimio yanayopitishwa yanatekelezwa kwa vitendo.