Wajasiriamali walia ukosefu mikopo asilimia 10 wamtwisha mzigo Dk Tulia

Mbeya. Mgombea  ubunge  Uyole  Dk Tulia Ackson  amesema  atashughulikia  kero ya ukosefu wa mikopo  asilimia 10 inayotolewa na halmashauri  kwa vikundi  vya wanawake ,vijana na watu wenye ulemavu.

Dk Tulia ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Oktoba 3,2025  wakati akiomba kura na kueleza utekelezaji  wa ilani ya uchaguzi 2025, 2030  kwa wananchi  wa Kata ya Mwakibete Mtaa wa Gerejini eneo la Soweto.

“Nimesikia kilio chenu kuna vikundi  waliomba mikopo wakapata, lakini wapo wengine wamefuatilia hawajapata naahidi hilo limekwisha nitafuatilia  cha msingi Oktoba 29, mwaka huu mkipigie kura Chama cha Mapinduzi  (CCM),ili kuweza kutatua cha changamoto zenu,” amesema.

Katika hatua nyingine  amesema atazungumza na uongozi  wa Jiji la Mbeya kuona uwezekano wa kutoa mikopo kwa kundi la vijana  watengeneza vyombo vya moto sambamba na kuwatengea  eneo rasmi na kuendesha shughuli  zao.

Dk Tulia amesema Serikali  inaendelea kutatua changamoto  za makundi  ya vijana na kutenge fedha kwa ajili ya kutoa mikopo katika makundi hayo na kwamba hivi karibuni  halmashauri  imetoa zaidi ya  Sh3.2 bilioni.

“Licha ya halmashauri  kutenga fedha za mikopo kila mwaka, lakini ndani ya siku 100 za mgombea  Urais Samia Suluhu Hassan  atamwaga mabilioni ya fedha kuwezesha makundi  hayo, jambo lenu ni moja tu Oktoba 29,mwaka huu ni kutiki, “amesema.

Wakati huo huo amehamasisha wananchi kutumia haki  ya kikatiba kujitokeza kupiga  kura za kishindo  kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Dk Tulia na Diwani Kata ya Mwakibete  Lucas  Mwampiki,” amesema.

Amesema namna pekee ya kutatuliwa changamoto  zenu ni kukipigia kura Chama cha Mapinduzi (CCM ) ili kusogezewa maendeleo  kwa wakati.

Diwani Kata ya Mwakibete, Lucas Mwampiki  amemuomba Dk Tulia kuboreshewa  miundombinu  ya elimu, barabara  ili kusaidia  jamii kunufaika  na miradi ya Serikali  ya awamu ya sita.

 Mwenyekiti  wa Umoja wa Wanawake (UWT), Mkoa wa Mbeya,  Edna Mwaigomole amemtaja Dk Tulia ni dawa ya wananchi wa Mbeya na  Uyole  hivyo ni jukumu la kila mmoja kupiga kura za kishindo  Oktoba 29, 2025.

“Tunataka kura nyingi za heshima  kwa Dk Tulia na Samia  ili tuweze kuletewa maendeleo  makubwa katika  majimbo ya Mbeya  mjini na Uyole,” amesema.

Mjasiriamali  wa mbogamboga  Soko la Soweto, Siwema Haule amesema changamoto kubwa ni ukosefu  wa mitaji na soko la kisasa na kumuomba mgombea  akipata ridhaa kuanza na changamoto  hizo.