Unguja. Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA), kwa kipindi cha robo ya kwanza, Julai hadi Septemba 2025 ya mwaka wa fedha 2025/2026, imefanikiwa kukusanya kwa ufanisi wa asilimia 100.08 miongoni kwa sababu zikitajwa ni kuimarisha mifumo na elimu kwa mlipakodi.
Katika kipindi hicho, Mamlaka ilikadiriwa kukusanya Sh274.073 bilioni ambapo kufikia Septemba 30, 2025 imefanikiwa kukusanya Jumla ya Sh274.292 bilioni.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ZRA kwa vyombo vya habari, Oktoba 3, 2025 imesema kwa ufanisi huu Mamlaka imeweza kuongeza kiwango cha makusanyo kwa wastani kwa mwezi kutoka Sh80 bilioni na kufikia wastani wa Sh90 bilioni.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, makusanyo haya, yanapolinganishwa na makusanyo halisi ya kipindi kama hiki kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kuna ongezeko la Sh73.357 bilioni, sawa na ukuaji wa asilimia 36.51 ambapo katika kipindi hicho, ZRA ilikusanya Sh200.935 bilioni.
Mkuu wa Kitengo cha habari, Uhusiano na Huduma kwa walipakodi, Makame Khamis Moh’d amesema ukuaji wa makusanyo ya kodi kwa asilimia 36.51 kwa kipindi cha Julai hadi Septemba 2025, pamoja na mambo mengine umesababishwa na kuimarika na kustawi kwa shughuli za kiuchumi kati ya Zanzibar na Tanzania Bara.
“Pia uwekezaji mkubwa katika ujenzi wa miundombinu na upanuzi wa huduma za kijamii ambazo zimesaidia kufungua fursa nyingi za kiuchumi ndani ya Zanzibar kufuatia utekelezaji wa sera nzuri za kiuchumi za Serikali ya Awamu ya nane,” amesema Makame
Makame ametaja sababu nyingine ni kuimarisha programu mbalimbali za elimu kwa walipakodi kunakopelekea kuwepo kwa ukaribu kati ya ZRA na walipakodi na hivyo kuchochea ulipaji wa kodi kwa hiari.
Pia ametaja sababu nyingine ni kuimarika kwa matumizi sahihi ya mifumo katika usimamizi wa kodi ikiwemo matumizi ya mfumo wa risiti za kielektroniki (VFMS), na matumizi ya mfumo wa ukusanyaji wa mapato wa ZIDRAS.
Kuongezeka kwa ufuatiliaji wa karibu wa walipakodi katika maeneo mbalimbali ya biashara kwa lengo la kuimarisha utoaji wa huduma za Kikodi na usimamiaji wa Weledi kwa kuongeza mafunzo kwa Wafanyakazi wa Mamlaka ambao unaochochea kuimarika kwa maadili na uwajibikaji.
Ili kuimarisha makusanyo kwa kipindi kijacho, ZRA imejipanga kusimamia kazi maalumu za ufuatiliaji wa walipakodi ikiwa ni pamoja na matumizi sahihi ya mfumo wa kutolea Risiti za Kielektroniki (VFMS) na uunganishaji wa Mifumo ya Teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) baina ya ZRA na biashara zinajiendesha kwa kutumia mifumo.
Baadhi ya wafanyabiashara kisiwani hapa wamesema utaratibu unaotumika kwa sasa ni mzuri tofauti na zamani kudai kodi yalikuwa yakitumika mabavu jambo ambalo liliwafanya kuonekana kuwa maadui
”Kwa sasa watendaji wanakuja kwenye biashara wanazungumza kauli nzuri tofauti na zamani ilionekana kama kuna uadui ukisikia wanakuja unafunga biashara, hivyo mazingira haya sishangai kusikia makusanyo yanaongezeka,” amesema Abdi Haji mfanyabiashara Mlandege