Ahukumiwa kifo kwa kuchapisha maneno ya kumkashifu Rais mitandaoni

Raia mmoja wa Tunisia, Saber Chouchane (56), amehukumiwa adhabu ya kifo kwa kosa la kuchapisha kwenye mtandao wa Facebook, maneno yanayodaiwa kumkashifu Rais Kais Saied na kudhalilisha vyombo vya usalama.

Hukumu hiyo ilitolewa jana Oktoba 3, 2025 na imekuwa gumzo nchini humo.

Mawakili wa Chouchane wamesema mtuhumiwa huyo ni mfanyakazi kibarua mwenye elimu ndogo, aliyekuwa akitoa maoni yake binafsi kupitia mitandao ya kijamii kabla ya kukamatwa mwaka jana.

“Hakimu wa Mahakama ya Nabeul, amemhukumu kifo kwa maneno aliyoyachapisha Facebook. Ni hukumu ya kushangaza na ambayo haijawahi kutokea,” amesema wakili wake, Oussama Bouthalja.

Hata hivyo, wakili huyo amebainisha kuwa tayari wamewasilisha rufaa kupinga uamuzi huo. Wizara ya Haki ya Tunisia haijatoa maelezo yoyote kufuatia hukumu hiyo.

“Hatuelewi kinachoendelea. Sisi ni familia masikini, na sasa tumepata maumivu ya kunyimwa haki juu ya umaskini wetu,” amesema mtuhumiwa, Jamal Chouchane.

Hukumu hiyo imezua mjadala mkubwa na ukosoaji mitandaoni, huku wanaharakati na wananchi wa kawaida wakionyesha kuchukizwa na kitendo hicho ambacho wanakitafsiri kama kuminywa uhuru wa kujieleza chini ya utawala wa Rais Saied.

Endelea kufuatilia Mwananchi