BALOZI NCHIMBI AMPONGEZA DKT. SAMIA KUIMARISHA UZALISHAJI WA KOROSHO LINDI,AMUOMBEA KURA WILAYANI NACHINGWEA.

MGOMBEA mwenza wa kiti cha urais kupitia Chama Cha Mapinduzi(CCM) Balozi Dkt.Emmanuel Nchimbi amesema kuimarika kwa Uzalishaji wa Korosho mkoa wa Lindi ni matokeo ya jitihada za Dk.Samia Suluhu Hassan kuweka mazingira mazuri, kuipa nguvu sekta ya kilimo kwa kuongeza wigo mpana kwenye ruzuku ya mbolea,mbegu na dawa.

Dkt Nchimbi ametoa kauli hiyo leo Septemba 03, 2025 alipokuwa akiwahutubia wananchi katika viwanja vya Maegesho, Kata ya Boma, Wilaya ya Nachingwea, mkoani Lindi,ikiwa ni muendelezo wa mikutano yake ya kampeni za Urais kuelekea Uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29,2025.

Akiwahutubia maelfu ya wananchi wa Nachingwea alipokuwa akinadi sera za CCM na kuomba kura,Dkt.Nchimbi amesema yote hayo yamewezekana ni kwasababu Rais Dk.Samia Suluhu Hassan aliweka kipaumbele kwenye sekta ya kilimo.

Ameongeza Dkt.Samia katika sekta ya kilimo ameongeza bajeti ya Wizara ya Kilimo kutoka Sh.bilioni 294 mwaka 2020 na kufikia zaidi ya trilioni moja mwaka 2024.

“Kingine ambacho nataka kusema hapa mazao ya Korosho katika mkoa wa Lindi yalipanda kutoka tani Elfu thelathini hadi kufikia tani elfu tisini ndani ya miaka minne ya utendaji kazi wa Dkt Samia Suluhu Hassan,”amesema.

Aidha baada ya kuwahutubia Wananchi hao,Dkt.Nchimbi pia alitumia nafasi hiyo kuwanadi baadhi ya wagombea Ubunge wa mkoa huo,akiwemo mgombea Ubunge wa Jimbo la Nachingwea,Ndugu Fadhili Ally Liwaka pamoja na Madiwani.

Dkt.Nchimbi anaendelea na mikutano yake ya hadhara ya kampeni nchini kote kusaka kura za ushindi wa kishindo za Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya CCM,Dkt.Samia Suluhu Hassan,Wabunge na Madiwani.

Pamoja na kuomba kura pia ameendelea kunadi  sera na Ilani ya chama hicho,iliyolenga kuboresha maisha ya Wananchi na maendeleo kwa ujumla,ambapo mpaka sasa amefika mkoa wa 17 tangu kuzinduliwa kwa kampeni hizo Agosti 28,2025 jijini Dar es Salaam.