Songwe. Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ismail Ali Ussi amewahimiza wananchi kulinda na kutunza miundombinu inayojengwa na Serikali kwa gharama kubwa, ikiwemo barabara na madaraja, akisisitiza kuwa ulinzi wa miundombinu hiyo ni muhimu kwa ustawi wa jamii na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
Ussi ametoa kauli hiyo Oktoba 4, 2025, baada ya kukagua na kuzindua daraja la mawe (box culvert) lenye midomo minne, lililojengwa katika barabara ya Mapogoro – Mtima, wilayani Ileje, mkoani Songwe.
Ameeleza kuwa daraja hilo ni sehemu ya mradi wa ujenzi wa barabara ya Mapogoro – Mtima yenye urefu wa kilometa mbili, ambayo inaunganishwa na barabara ya Mlale – Ikumbilo yenye urefu wa kilometa 14.
Mradi huo unatekelezwa na kampuni ya Ngongo and Sons Construction Limited kutoka wilayani Mbozi.
Kwa mujibu wa Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) Wilaya ya Ileje, Mhandisi Lugano Mwambingu, ujenzi wa daraja hilo ulianza Agosti 29, 2024, na kukamilika Mei 29, 2025, kwa gharama ya Sh59.5 milioni zilizotolewa kupitia Mfuko wa Barabara (Road Fund).
Mhandisi Mwambingu amesema daraja hilo limekamilika kwa asilimia 100 na tayari limeanza kutumika, likiwaunganisha wakazi wa vijiji vya Mapogoro na Mtima, na kurahisisha upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii ikiwemo shule, zahanati na masoko.
“Mbali na kurahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa, daraja hili limejengwa pia kama ‘relief culvert’ ili kulinda miundombinu ya barabara ambayo mara kadhaa ilikuwa ikiharibiwa na mafuriko,” amesema Mhandisi Mwambingu.
Amebainisha kuwa mradi huo pia umechangia kutoa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kwa wananchi, hivyo kuongeza kipato na ustawi wa jamii.
Kwa niaba ya wananchi, Mhandisi Mwambingu amemshukuru Rais, Dk Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kupeleka fedha nyingi katika sekta ya barabara, akisisitiza kuwa miradi kama hiyo inazidi kufungua fursa za kiuchumi katika wilaya ya Ileje.
Stephania Panja, mkazi wa Kijiji cha Mtima, amesema eneo hilo hapo awali lilikuwa na changamoto kubwa, hasa wakati wa msimu wa mvua, ambapo wananchi walishindwa kuvuka kutokana na maji mengi yaliyokuwa yakijaa na kuwa hatari kwa watoto pamoja na watu wazima.
“Eneo lilipojengwa daraja hilo watu walikuwa wakinusurika kifo kwa kuzama maji, hivyo wanaishukuru serikali kwa kufanikisha ujenzi wa karavati hilo kuwaondolea adha wananchi,” amesema Panja.