YANGA haiwafurahishi baadhi ya mashabiki wake kutokana na soka ambalo wanalitaka, lakini kikosi kinaendelea kupata matokeo mazuri uwanjani kikiwa chini ya kocha Romain Folz.
Kuna mabadiliko matano ambayo Yanga chini ya Folz imeyaonyesha tangu kocha huyo aanze kuifundisha akiichukua kutoka kwa Mfaransa mwenzake Hamdi Miloud aliyetimkia Ismaily ya Misri.
Hebu tuangalie mambo matano ambayo yameibuka kuwa mabadiliko kwenye Yanga ya Folz ambaye alitua nchini Julai 9, 2025 kwenye mechi nne za mashindano ilizocheza mpaka sasa. Zingatia baadhi ya mambo kwa makocha wengi wa karibuni walipita na hawakuyafanya.
Yanga chini ya Folz imerejesha heshima ya nahodha mkuu wa timu hiyo, Bakari Mwamnyeto ambaye amerudi uwanjani akiwa kama yule aliyetua klabuni hapo akitokea Coastal Union ya Tanga miaka mitano iliyopita.
Ingawa Folz hajaweka wazi, lakini Mwanaspoti linafahamu kuwa kocha huyo beki chaguo lake namba moja ni Mwamnyeto kati ya watano alionao kikosini.
Kwa muda mrefu Yanga eneo la kati limekuwa kwenye miliki ya nahodha msaidizi Dickson Job na Ibrahim Hamad ‘Bacca’ ambao pia wamejibeba mpaka Taifa Stars wakicheza pamoja.
Job na Bacca walimuondoa Mwamnyeto Stars na hata ndani ya kikosi cha Yanga kwa kuwa chaguo la kwanza chini ya makocha wote wanne waliopita kuanzia Nasreddine Nabi, Miguel Gamondi, Sead Ramovic na Hamdi Miloud.
Utawala wa Job na Bacca ulimuweka Mwamnyeto benchi muda mrefu akipata nafasi ndogo ya kuanza iliyoweka wasiwasi juu ya hatima yake.
Hata hivyo, chini ya Folz, Mwamnyeto halisi amerejea akirudisha nafasi yake, ubora wake akiwa ameshaanza kwenye mechi mbili dhidi ya Wiliete ugenini mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini pia mchezo wa kwanza wa Ligi msimu huu dhidi ya Pamba Jiji.
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya Yanga ni kwamba Mwamnyeto ilibaki kidogo kuanza pia kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba, lakini kuna mazungumzo yakabadili mpango huo.

Yanga kipindi cha pili haikuachi
Kitu ambacho baadhi ya mashabiki wa Yanga wanakililia ni timu kutocheza soka la kuvutia, lakini Folz anawabana sehemu moja tu – hakuna mpinzani aliyetoka salama. Folz kwenye mechi nne amepangua mziki wake akionyesha kumpa nafasi mchezaji yeyote anayemuona yupo tayari kucheza akiwa na ‘rotesheni’ kubwa, lakini kitu muhimu timu yake imepata matokeo.
Kwenye mechi nne ambazo Yanga achana na kushinda zote, lakini mechi tatu imetengeneza ushindi wake kwenye kipindi cha pili ambacho huwa inarudi na nguvu kubwa.
Mechi dhidi ya Simba, Pamba Jiji na Wiliete ikiwa nyumbani zote Yanga imetengeneza ushindi wake kipindi cha pili ambacho imefunga mabao saba katika mabao nane iliyofunga ndani ya mechi nne za mashindano, huku mchezo wa kwanza ugenini dhidi ya Waangola hao ndio ilifunga bao moja katika kipindi cha kwanza.

Hakuna ambaye alitangulia kufikiria kwamba presha ya usajili wa kiungo Moussa Bala Conte wakati anatua Jangwani, lakini kwa sasa anaweza kusota benchi huku kiungo kutoka Kyela, Mbeya, Aziz Andabwile ambaye alitokea Fountain Gate akachukua nafasi.
Andabwile amepindua meza akianza kwenye mechi tatu akipewa imani na Folz kisha akaitendea haki akiwa chaguo la kwanza kucheza mbele ya mabeki wa kati wa timu hiyo ilhali Conte akisubiri nje.
Jambo muhimu zaidi ukicha ubora wa kucheza eneo la kati ambalo Andabwile ameonyesha ubora akajiongeza akifunga mabao mawili kwenye mechi mbili tofauti, lakini hatua hiyo imemfanya kuuteka moyo wa Folz.
Boyeli subiri, Dube twende
Wakati Folz anatua Yanga usajili wake wa kwanza ulikuwa ni kumbeba mshambuliaji Andy Boyeli, lakini hata hivyo hajawa mnafiki pengine kwa kutorishwa na kiwango chake na hivyo amemtupa jukwaani Mkongomani huyo huku chaguo lake la kwanza likibaki kuwa ni Prince Dube. Boyeli ameanza kwenye mechi moja akiwa hana bao akibaki na asisti moja wakati Dube akifunga bao katika mechi tatu alizoanza huku moja akitokea benchi.

Mpaka sasa Yanga chini ya Folz haijaruhusu bao huku kwenye ukuta wake ikionyesha kuwa na utulivu mkubwa licha ya mabadiliko ya kikosi. Ukiacha ubora huo wa ukuta pia kule mbele nako mambo mazuri timu yake ikifunga mabao ambapo mpaka sasa imeshatupia manane kwenye mechi nne za mashindano.
Mchezo mmoja pekee tena dhidi ya Simba ndio kikosi hicho kilitoka na ushindi wa bao 1-0, lakini mingine yote kikipata ushindi wa kuanzia mabao mawili na kuendelea. Acha tuendelea kuangalia mabadiliko zaidi ya Folz pale Jangwani.