Halmashauri kufungua kiwanda cha parachichi, kituo cha mafunzo kwa vijana

Mbeya. Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya imetangaza mpango wa kufungua kiwanda cha kuchakata parachichi, kwa lengo la kuwasaidia wakulima kuuza mazao yao kwa uhakika na kwa bei nzuri, pamoja na kufungua fursa za ajira kwa vijana.

Kupitia kituo cha mafunzo cha Iposa, vijana watapatiwa mafunzo mbalimbali ya fani, yatakayowawezesha kujiajiri na hata kuwaajiri wengine, hivyo kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira katika wilaya hiyo.

Halmashauri imesisitiza kuwa mradi huu utakuwa kichocheo kikubwa cha kuinua kilimo cha parachichi na kuinua maisha ya wakulima na wananchi kwa ujumla.

Mbali na zao la parachichi, Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya imesema imepanga kuandaa mpango wa muda mrefu wa maendeleo ya kilimo kwa kipindi cha miaka 10 hadi 100, ili kuendeleza sekta hiyo kiuchumi kwa kutumia fursa zilizopo kwenye mazao mbalimbali yakiwemo pareto, viazi mviringo, kahawa, maharage na mahindi.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Erica Yegella akizungumza ofisini kwake



Akizungumza leo Jumamosi, Oktoba 4, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Erica Yegella, amesema tayari halmashauri inamiliki shamba lenye ukubwa wa ekari 500 lililoandaliwa na watangulizi wake, na sasa kuna mpango wa kulifufua na kuliboresha kwa ajili ya kuanzisha kilimo cha kisasa cha parachichi na mazao mengine.

“Lengo letu si parachichi pekee, bali kutumia rasilimali tulizonazo kuimarisha kilimo kwa ujumla.

“Tunaamini kupitia kampuni ya halmashauri iliyosajiliwa, tuna uwezo wa kuanzisha viwanda vya kuchakata mazao kama mahindi, pareto, viazi, maharage na kahawa ili kuongeza thamani na kuinua kipato cha wananchi wetu,” amesema Yegella.

Ameongeza kuwa hatua hizo ni sehemu ya mkakati wa halmashauri wa kufungua ajira kwa vijana na kuchochea uchumi wa ndani kwa kutumia kilimo kama mhimili mkuu wa maendeleo endelevu.

“Kwa maana hiyo, wakulima wa parachichi wataweza kuuza zao kwenye kiwanda hicho, lakini itafungua fursa ya ajira kwa vijana wenye uwezo na elimu, halmashauri yetu inazo tunu nyingi ambazo kila mmoja anaweza kuishi maisha mazuri,” amesema Erica.

Mkurugenzi huyo amesema katika kuwapigania vijana wenye wenye elimu ambao walikosa ajira, aliamua kukutana nao kwenye makongamano kuwapa elimu ambapo kwa sasa anajivunia kuvuna baadhi wanaojitegemea kwa nafasi mbalimbali.

Amesema mbali na kukutana nao kwenye mikutano na kongamano, halmashauri hiyo imeamua kuweka kituo maalumu cha Iposa ambacho kinatoa elimu ya ujasiriamali kwa ajili ya kuwakwamua vijana kujiajiri na kuajiri wengine.

“Katika kituo hicho vijana wanafundishwa fani mbalimbali kwa maisha yao ya baadaye na tunafikiria kuongeza kozi nyingine na matarajio yetu ni kuandaa kongamano la pamoja ili kuwakutanisha kama sehemu ya mafanikio kwa halmashauri.

“Tupo kwenye mpango wa kuwafundisha mfumo wa manunuzi ‘Nest’, ili wawe washindani kupitia mafunzo waliyopata wapate miradi ya Serikali, hadi sasa vijana 500 wamefuzu na wengine wanaendelea na masomo,” amesema Erica.

Hata hivyo, mkurugenzi huyo hakusita kuwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye mapokezi ya mwenge wa uhuru ambao utapokelewa wilayani humo Oktoba 9, ukitarajia kukagua na kuzindua miradi ya Sh1.3 bilioni.

Mkulima Jesca Mwashilindi amesema kwa sasa mazao hayana bei rasmi kutokana na kukosa uhakika wa soko, ambapo uwapo wa kiwanda cha parachichi na mengine yanaweza kuamsha uchumi wa wakulima.

“Kilimo ndio uti wa mgongo kila binadamu lazima ale ili aishi, lakini sehemu ya bei halisi ya mazao yetu tunalima hatujui tutauza wapi, hivyo nimpongeze mkurugenzi kwa fikra hizo ambazo zinaweza kututoa kiuchumi,” amesema Jesca.

Naye Rebeca Mwampashi amesema kilio cha wakulima si mashamba kwa sasa wala mbolea, bali wanahitaji uhakika wa soko kwa kuwa wanalima kwa ajili ya biashara, lakini hawaelewi hatma yao.

“Tuna mazao mengi yanayostawi hapa Mbeya Vijijini, serikali ilishatupa mbolea, sasa tunahitaji soko la uhakika, lakini suala la ajira kwa vijana tunaona mipango ya Mkurugenzi wetu amelipa uzito kwa kubuni mbinu kuwasaidia,” amesema Rebeca.