UONGOZI wa Fountain Gate umesema hautafanya uamuzi wa haraka kutafuta kocha mkuu, badala yake Mohamed Ismail ‘Laizer’ ambaye ni msaidizi atapewa majukumu ya kukiongoza kikosi hicho katika kipindi cha mpito.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mratibu wa Fountain Gate, Wendo Makau amesema baada ya kuondoka Denis Kitambi hawana haraka ya kutafuta mkuu wa benchi la ufundi, hivyo Laizer ataongoza kikosi kwa muda.
“Hatuhitaji tena kufanya haraka ya kusuka benchi la ufundi kwa sababu tutaendelea kuivuruga timu tena baada ya kuondoka kwa Kitambi, Laizer ndiye atayeongoza akishirikiana kwa ukaribu na Abubakary Ally aliyekuwa kwa vijana,” amesema Wendo
Amesema kinachoendelea ni kutatua changamoto ya wachezaji walioshindwa kucheza kutokana na kutoingia katika mfumo wa usajili kwa wakati huku wakiwa na matumaini kila kitu kitakamilika kabla ya Ligi Kuu kurejea Oktoba 17.

Kitambi mwenye uzoefu na soka la Tanzania amefundisha Simba, Namungo, Geita Gold na Singida Black Stars ambapo aliachana na Fountain Septemba 28, 2025 kwa makubaliano.
Kitambi alijiunga na kikosi hicho kwa ajili ya kuchukua nafasi ya Mnigeria, Ortega Deniran, aliyeondoka mapema tu kabla ya msimu wa 2025-2026 kuanza na kumuachia kocha huyo ambaye hata hivyo, aliiongoza katika mechi mbili za Ligi Kuu Bara.

Baada ya kuondoka Ortega, Kitambi aliiongoza Fountain Gate katika mechi mbili za Ligi Kuu Bara na kupoteza zote, ambapo alichapwa kwa bao 1-0, dhidi ya Mbeya City Septemba 18, 2025, kisha kuchapwa tena mabao 3-0 na Simba, Septemba 25, 2025.
Kuondoka kwa Kitambi kunamfanya Laizer aliyeinusuru na janga la kushuka daraja msimu akaanza kwa kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar, Septemba 28, 2025, ikiwa ni mechi ya kwanza ya Ligi Kuu kuongoza akiwa kocha mkuu msimu huu.