AL Merrikh ya Sudan imetupwa nje katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kulazimishwa suluhu nyumbani na FC Lupopo ya DR Congo.
Katika mechi ya kwanza iliyopigwa wiki iliyopita huko DR Congo, Al Merrikh ilipoteza kwa bao 1-0 na hivyo kuifanya FC Lupopo kutinga raundi ya pili ya michuano hiyo na sasa itavaana na Orlando Pirates ya Afrika Kusini.
Hii ni timu ya tatu ya DR Congo kwa siku ya leo Jumamosi kufanya kweli katika mechi zao za vipo vya CAF baada ya Simba na As Maniema Union kufanya kweli katika mechi za Kombe la Shirikisho Afrika.
Kwa sasa imesalia mechi moja tu ya kiporo cha raundi kwa kwanza kati ya APR ya Rwanda itakayoifuata Pyramids ya Misri kesho, huku ikiwa na deni la kipigo cha nyumbani cha mabao 2-0 yote yakifungwa na nyota wa zamani wa Yanga na AS Vita, Fiston Mayele. .
Katika michuano ya Kombe la Shirikisho AS Maniema ya DR Congo imesonga mbele baada ya kulazimisha sare ya 2-2 ugenini dhidi ya Pamplemousses ya Mauritius na kusonga kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-2, kwani mechi ya kwanza ikiwa nyumbani ilishinda 2-1.
Nayo Simba imeifunga Djabal ya Comoro kwa mabao 2-0 na kutinga raundi ya pili kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-0.