Shinyanga. Katika maisha ya kila siku ya wazazi, hasa wanapokuwa wakibadilisha nepi za watoto, kutumia taulo laini ‘baby wipes’ ni jambo la kawaida.
Ni rahisi, haraka na hutoa unafuu, hasa pale maji yanapokuwa hayapatikani kwa urahisi. Lakini nyuma ya urahisi huo kuna tahadhari inayotolewa na wataalamu wa afya.
Kwa mujibu wa wataalamu hao, licha ya faida za matumizi ya taulo hizo, vilevile zinaweza kusababisha michubuko na muwasho wa ngozi, kwani baadhi huwa na harufu ya manukato, kileo au kemikali zingine zinazoweza kusababisha ngozi ya mtoto kuwa nyekundu au kuwasha.
Si hivyo pekee, wapo wanaopatwa na upele kutokana na uwepo wa viambato vyenye kemikali, pia mzio. Inaelezwa iwapo ‘wipes’ hazitahifadhiwa vizuri zikapoteza unyevu na kupata fangasi, zinaweza kusababisha maambukizi kwenye ngozi ya mtoto.
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, ni muhimu kutumia taulo hizo kwa umakini hasa kwa watoto wachanga chini ya miezi sita kwani wana ngozi nyororo zaidi, pamoja na wale wenye historia ya ngozi yenye kuathiriwa kwa urahisi.
Rose Njemu na Khadija Suleiman, wakazi wa Shinyanga mjini ni sehemu ya kundi kubwa la wazazi wanaotumia taulo hizo kwa usafi wa watoto wao.
Rose anasema huzitumia kwa kuwa humrahisishia usafi wa mtoto, hasa awapo safarini na katika mazingira ambayo maji ni adimu.
“Wipes husaidia wakati wa safari ndefu, pia katika mazingira ambayo upatikanaji wa maji ni wa shida. Wakati mwingine hata watu wazima tunazitumia,” anasema.
Kwa upande wake, Khadija anasimulia alizitumia kwa takribani miezi miwili, mtoto akapata upele sehemu za siri, awali akahisi ni kutokana na joto.
“Kadri siku zilivyosogea upele ukazidi, nilipompeleka hospitali madaktari wakagundua ni kemikali zilizopo kwenye ‘baby wipes’ nikashauriwa niache kuzitumia. Nikawa natumia kitambaa safi cha kawaida kumfuta mtoto,” anasema.
David Mfula, daktari kutoka Idara ya Watoto, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, katika mahojiano na Mwananchi anasema taulo hizo hutengenezwa viwandani zikiwa na kemikali zinazoweza kuleta madhara kwa ngozi ya mtoto.
“Kemikali huua bakteria wazuri wanaolinda ngozi ya mtoto, hivyo kuongeza hatari ya maambukizi ya magonjwa mengine na kusababisha mtoto kupata upele, muwasho na michubuko. Taulo hizi zinaweza kusababisha mtoto kupata mzio kutokana na viambato kama paraben, phenoxyethanol, methylisothiazolinone (MIT)” anasema.
Anasema dalili za mzio ni ngozi kuwa nyekundu, kuwasha, vidonda vidogovidogo, ngozi kukauka au kupasuka.
Dk Mfula anasema tangu Januari 2025 hadi Septemba, wamepokea watoto watano hospitalini hapo waliopata madhara yatokanayo na matumizi ya taulo hizo.
Katika kuwahudumia anasema: “Kwanza tunachunguza chanzo cha ugonjwa, kisha tunamshauri mzazi kuacha kuzitumia (wipes), badala yake watumie kitambaa cha kawaida ambacho ni salama kumfutia mtoto. Ugonjwa ukizidi tunatoa dawa ambazo ni anti-allergy ambazo hutolewa bila malipo.”
Pamoja na hayo, wataalamu wanashauri kutumia taulo zisizo na harufu za manukato wala kileo, pia zenye alama “hypoallergenic” (zisizo rahisi kusababisha mzio).
Vilevile, kuepuka kuzitumia mara kwa mara, badala yake yatumike majisafi na kitambaa laini cha pamba. Inasisitizwa kuchunguza ngozi ya mtoto na iwapo itaonyesha wekundu au vipele, basi taulo hizo zisitumike.
Gladness Mutajunwa, daktari kutoka idara ya watoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, anasema unaponunua wipes unapaswa kuangalia viambato vilivyotumika kuzitengeneza.
“Unatakiwa kuangalia wipes zenye viambato vya asili kama aloe vera, chamomile au majisafi ambazo ni bora kwa watoto wachanga, pia zisizo rahisi kusababisha mzio (hypoallergenic). Ni bora zaidi kama zimefanyiwa majaribio ya dematolojia,” anasema.
Amesema taulo hizo zinapaswa kuwa na unyevu wa kutosha ili kusafisha vizuri pasipo kutumia nguvu, lakini si za kulowesha sana. Ziwe nzito zisizokatika kirahisi na zenye muundo kama mistari kwani husaidia kusafisha vizuri zaidi.
“Mzazi anatakiwa kuchagua wipes zisizo na harufu hasa kwa watoto wachanga au ahakikishe ni harufu ya asili na si kali, pia zilizo katika kifungashio kinachofungika vizuri ili kudumisha unyevu,” anasema akieleza zilizo na kifuniko cha plastiki ni bora kuliko zenye stika pekee.
Dk Gladness anashauri maji na kitambaa safi kutumika kumsafisha mtoto ikiwa ni mbadala wa wipes kwani hazina kemikali ya aina yoyote,
“Tumia maji ya uvuguvugu na kitambaa laini cha pamba hii ni salama kwa ngozi, haina kemikali na ni ya bei nafuu. Kitambaa kinaweza kufuliwa na kutumika tena,” anasema.