Mbio za baiskeli kutumika kurudisha tabasamu kwa wanafunzi Dodoma

Dodoma. Ili kuchangia upatikanaji wa elimu bora kwa wanafunzi wanaotoka katika mazingira magumu, Shule ya Spring Hill Academy imeandaa mbio maalumu za baiskeli kwa ajili ya kukusanya fedha zitakazotumika kusaidia watoto hao.

Akizungumza leo, Jumamosi Oktoba 4, 2025, Meneja wa Spring Hill Academy, Careen Billington amesema mbio hizo zinatarajiwa kufanyika Novemba 29 katika barabara za Mji wa Serikali, Mtumba, jijini Dodoma.

Billington amesema lengo la tukio hilo ni kukusanya Sh100 milioni ambazo zitatumika kununua mahitaji ya shule kwa wanafunzi kutoka familia zisizo na uwezo, wanaosoma katika shule za serikali.

“Watoto hawa wanakabiliwa na changamoto nyingi zinazowazuia kufikia ndoto zao. Kupitia mbio hizi, tunalenga kuwapa msaada wa vifaa vya shule ili waweze kujifunza kwa ufanisi zaidi,” amesema.

Amewahamasisha wadau mbalimbali kushiriki au kuchangia ili kuhakikisha lengo hilo linafanikiwa na kuwa chachu ya mabadiliko chanya kwa maisha ya watoto hao.

“Hizi mbio zitalenga kukusanya fedha kwa ajili za kuwapatia misaada wanafunzi wanaotoka kwenye familia duni zenye kipato cha chini ili wamalize masomo yao na kupata elimu bora,” amesema Careen.

Careen ameongeza kuwa, miongoni mwa misaada watakayoitoa ni sare za shule na viatu, madaftari kalamu na kuwalipia ada baadhi ya wanafunzi ili kuwapa nafasi ya kumaliza masomo yao bila changamoto.

Balozi wa Shule ya Spring Hill Academy, Imanueli Matias ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki au kuchangia kwa njia mbalimbali ili kufanikisha malengo ya kampeni hiyo, ambayo inalenga siyo tu kusaidia watoto wa mazingira magumu, bali pia kuimarisha mshikamano na moyo wa kusaidiana miongoni mwa Watanzania.

Matias amesema kuwa kampeni hiyo ni zaidi ya tukio la kuchangisha fedha, kwani inaleta pamoja jamii katika juhudi za kuboresha maisha ya watoto ambao wanategemea elimu kama njia pekee ya kujinasua kutoka kwenye umaskini.

“Kila mchango una maana. Kwa pamoja tunaweza kubadilisha maisha ya watoto hawa na kuwapa nafasi ya kufikia ndoto zao,” amesema Matias.

Hatua hi pia imeungwa mkono na wadau wa elimu pamoja na wanajamii, ambao wamesema jitihada hizi ni mfano mzuri wa sekta binafsi kushirikiana na jamii katika kutatua changamoto za elimu badala ya kuiachia Serikali pekee.

Wameongeza kuwa jitihada  hizi pia  zinaonyesha namna ambavyo michezo inaweza kuwa chachu ya mabadiliko chanya katika jamii badala ya kutumika kama sehemu ya kutoa burudani pekee.