Moshi. Mrajisi wa vyama vya ushirika nchini, Dk Benson Ndiege amewataka wadau wa sekta ya kahawa nchini kuongeza ubunifu katika eneo la masoko ili kuongeza thamani na matumizi ya kahawa ya Tanzania duniani.
Akizungumza leo Oktoba 4, 2025 wakati wa uzinduzi wa Tamasha la Kahawa (Kahawa Festival) msimu wa sita, linalofanyika kwa siku tatu mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, Dk Ndiege amesema ni muhimu kutumia fursa hiyo kuhamasisha matumizi ya kahawa ya ndani ili kuongeza kipato cha wakulima wa zao hilo.
Amesema duniani kote takribani vikombe bilioni tatu vya kahawa hunywewa kila siku, lakini kwa Tanzania ni asilimia saba pekee ya kahawa inayozalishwa ndiyo inatumika nchini na hivyo kusisitiza umuhimu wa watanzania kujenga utamaduni wa kunywa kahawa ili kuongeza soko la ndani na nje nchi.
“Tusaidieni kuwa wabunifu kwenye eneo la masoko na tusiishie kufikiria minada pekee, najua KNCU au KDCU mnaingia kwenye minada, tunanunua kahawa tunapeleka nje, lakini sasa tujikite kwenye ubunifu zaidi na kuhamasisha soko la ndani na uandaaji wa kahawa nzuri.
“Wageni wanapokuja nchini wanapaswa kukutana na kahawa bora ya Tanzania katika maeneo yote watakayopita, hii ni fursa ya kujitangaza,” amesema Dk Ndiege.

Mrajisi wa vyama vya ushirika nchini, Dk Benson Ndiege (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa tamasha la kahawa(Kahawa festival) msimu wa sita.
Amesisitiza vyama vya ushirika kuhakikisha wakulima wanapata elimu ya kilimo chenye tija na kutumia maofisa ugani kwa ufanisi ili kuongeza uzalishaji.
“Serikali inatambua umuhimu wa kilimo kwani zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wanahusika moja kwa moja na sekta hiyo, bajeti ya kilimo imekuwa ikiongezeka kila mwaka, hivyo wakulima wachangamkie fursa ya miche milioni 20 ya kisasa inayotolewa bure na Bodi ya Kahawa ili kuongeza uzalishaji,” amesema.
Kwa mujibu wa Dk Ndiege, uzalishaji wa kahawa Kanda ya Kaskazini umeongezeka kutoka tani 8,000 mwaka 2020 hadi tani 12,000 mwaka huu, akibainisha kuwa bado kuna haja ya kuongeza juhudi zaidi ili kurejesha hadhi ya zao hilo katika mikoa ya kanda hiyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Kahawa Tanzania, Profesa Aurelia Kamuzora amesema zao la kahawa limeendelea kuwa nguzo kuu ya uchumi kwa taifa na familia nyingi nchini.
“Leo tunatembea kifua mbele tukijivunia kwamba kahawa ndiyo injini ya uchumi katika mikoa inayolima zao hili. Kwa miaka mingi, kahawa imekuwa chanzo kikubwa cha mapato na maendeleo ya jamii,” amesema Profesa Kamuzora.
Ameongeza kuwa Kahawa Festival 2025 inalenga kuongeza ushirikiano na kujenga mnyororo wa thamani wa sekta hiyo huku wadau wakijifunza mbinu mpya za uzalishaji na masoko.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), Primus Kimaryo amesema tamasha hilo limekuwa chachu ya kuunganisha wadau wote katika mnyororo wa thamani ya kahawa kuanzia shambani hadi sokoni.
“Nchi yetu inapokea wageni wengi kutoka maeneo mbalimbali. Wanapofika hotelini, maduka makubwa au migahawani, wanakuta kahawa ya Tanzania. Tuliona ni muhimu kila mmoja katika mnyororo huu mkulima, mfanyabiashara na taasisi kuelewa anachokifanya na ubora wa kahawa anayozalisha au kuuza,” amesema Kimaryo.
Ameongeza kuwa tamasha hilo ambalo sasa linafanyika kwa msimu wa sita mfululizo, limechangia kwa kiasi kikubwa kukuza utambulisho wa kahawa ya Tanzania katika soko la kimataifa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Kahawa Festival, Dennis Mahulu amesema maadhimisho ya mwaka huu yamepata mwitikio mkubwa kutoka kwa washiriki ambao wameongezeka kutoka mashirika 20 mwaka jana hadi 50 mwaka huu.
“Kwa siku tatu tutakuwa na maonyesho yatakayofungua fursa mpya katika sekta ya kahawa. Wakulima watapata nafasi ya kujifunza kuhusu masoko, ubora, na sheria mpya za Umoja wa Ulaya zinazohimiza uzalishaji unaolinda mazingira,” amesema Dennis.
Ameongeza kuwa lengo ni kuhakikisha wakulima wote wanaingia kwenye mfumo wa kidijitali wa uzalishaji wa kahawa ili kuendana na mahitaji ya soko la kimataifa.
“Sekta binafsi na serikali lazima tushirikiane kuhakikisha kahawa ya Tanzania inaendelea kung’ara duniani kkte,” amesema Mahulu.