Zaidi ya nyota 150 wa mchezo wa gofu kutoka mataifa matano ya Afrika, wameendelea kuchuana vikali kwenye mashindano ya wazi ya Tanzania Open 2025 yanayofanyika katika viwanja vya Kili Golf, wilayani Arumeru mkoani Arusha.
Wachezaji hao wanatokea Tanzania, Kenya, Rwanda, Burundi na Zambia, huku wakipambana kwenye mashimo 72 kwa siku nne mfululizo kuanzia Oktoba 2, 2025, ambapo michuano hiyo inatarajiwa kufikia tamati kesho Jumapili, Oktoba 5, 2025.
Mwenyekiti wa Chama cha Gofu Tanzania (TGU), Gilman Kasiga, amesema mwaka huu wameshirikisha makundi mbalimbali yakiwemo wachezaji wa kulipwa, ridhaa na pia watoto kwa wanawake na wanaume.
“Wadhamini wengi wamejitokeza mwaka huu na hii ni hatua kubwa, kwani ni matokeo ya uaminifu wetu, ndiyo maana sasa wadau wanavutiwa kushiriki na kuendeleza mchezo huu,” amesema Kasiga.

Nguvu Kamando, Mkurugenzi wa Vodacom Biashara ambao ni wadhamini wakuu wa mashindano hayo kwa mwaka wa tatu mfululizo, amesema lengo lao ni kuboresha maisha ya Watanzania kupitia michezo na teknolojia.
“Tunafurahi kuwa sehemu ya mashindano haya, gofu si burudani pekee bali pia ni mchezo unaowaunganisha watu wa rika na taaluma tofuati kubadilishana mawazo,” amesema Kamando.
Elinisaidie Msuri, Mkurugenzi wa HLB Tanzania, amesema ushiriki wao wa kwanza kwenye mashindano hayo ni mwanzo wa kushirikiana na TGU kuhakikisha gofu inasonga mbele nchini.
Kwa upande wake Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Arusha, Witness Shoo, amesema TANAPA katika kutambua umuhimu wa mchezo huo katika kutangaza utalii imejenga uwanja wa gofu katika mbuga ya Serengeti ili kutoa nafasi kwa mashindano makubwa zaidi ya kimataifa kufanyika hapa nchini.

“Matumaini yetu ni kuona mashindano yajayo yakifanyika Serengeti, tukitimiza kauli mbiu yetu ya ‘Tunatalii na Gofu,’” amesema Shoo.
Naye Ngumo Kingori, mchezaji wa kulipwa kutoka Kenya, amesema mbali na ushindani mkali, gofu kwake ni nafasi ya kukutana na watu mbalimbali, kubadilishana mawazo na pia kuboresha mwili kupitia mazoezi.