Rajoelina: Kizazi Gen-Z kilichompa madaraka sasa kinamtaka ang’atuke

Dar es Salaam. Kuna msemo wa Kiswahili, ‘utavuna ulichopanda’ ndivyo ilivyo kwa Rais Andry Rajoelina wa Madagascar ambaye ametoa kauli ya kukosoa maandamano ya Gen-Z dhidi ya Serikali yake.

Ni maandamano ya kizazi cha Gen-Z yaliyoanza Septemba 25, 2025, wakipinga ukosefu wa huduma za uhakika za umeme na maji.

Hata hivyo, madai hayo yaliongezeka kadiri siku zilivyoenda, ambapo waandamanaji sasa wanataka mabadiliko makubwa ya kisiasa, ikiwa ni pamoja na kujiuzulu kwa Rais Rajoelina.

Rajoelina ambaye mwaka 2009 akiwa meya aliingia madarakani kwa kuongoza maandamano yaliyomng’oa madarakani Rais wa wakati huo, Marc Ravalomanana.

Juzi Rajoelina ametoa kauli kuwa “kukosoa matatizo yaliyopo si lazima kuonyeshwa mitaani,” akijibu maandamano yanayoongozwa na kizazi cha Gen-Z dhidi ya serikali yake, ambayo sasa yameingia siku ya 10 tangu yaanze, huku waandamanaji kadhaa wakiripotiwa kuuawa na wengine kujeruhiwa.


Hata hivyo, Gen-Z Gen-Z nao wamemjibu; “Sisi ndio tumaini la mwisho,” wakiapa kuendelea kupaza sauti zao kwa maanadamano hadi Rais Rajoelina ajiuzulu.

Pamoja na Rajoelina kuvunja Serikali yake kwa kumfukuza kazi waziri mkuu, bado Gen-Z wamedai yafanyike mabadiliko zaidi ikiwamo Rais mwenyewe ajiuzulu.

Licha ya kuyashutumu maandamano ya sasa, Rajoelina naye alikuwa kama Gen-Z wa wakati wake.

Akiwa na umri wa miaka 34 na kushika wadhifa wa Meya wa Jiji la Antananarivo, aliongoza maandamano mwaka 2009 yaliyosababisha mapinduzi ya kijeshi na kumuondoa madarakani Rais wa wakati huo, Marc Ravalomanana.

Rajoelina aliyekuwa DJ kwenye kumbi za starehe na vilabu vya usiku, alitumia wadhifa wake wa meya na vyombo vyake binafsi vya habari (radio na televisheni) kupinga ufisadi, ukosefu wa huduma bora, na utawala wa mabavu wa Ravalomanana.

Tofauti na njia aliyoitumia yeye (Rajoelina) kuhamasisha maandamano kuipinga Serikali ya Ravalomanana, Gen-Z wa sasa wametutumia maendeleo ya teknolojia kufikishiana ujumbe.

Kilichofanywa na Gen-Z wa sasa, wametumia mitandao ya kijamii kama Facebook na TikTok kufikishiana ujumbe wa maandamano ambao ulifika hadi makundi mengine ya asasi za kiraia na wanasiasa wa ndani.

Hata hivyo, Rajoelina amekuwa wa kisasa zaidi kwa kuweka video aliyojirejodi kwenye ukurasa wake wa Facebook akilenga kuwafikishia ujumbe Gen-Z kwamba “wanatumiwa kuchochea mapinduzi.”

Pia, Rajoelina alinukuliwa akisema; “kukosoa matatizo yaliyopo si lazima kuonyeshwa mitaani; inapaswa kufanywa kupitia mazungumzo.” Kauli ambayo ni tata ikilinganishwa nay eye alivyoendesha siasa zake akiwa meya hadi kuingia madarakani.

Akiwa na umri wa 34 tu, Rajoelina alikabidhiwa rasmi madaraka ya urais tarehe 21 Machi 2009, na hivyo kuwa rais mdogo zaidi Afrika wakati huo.

Rajoelina alianza kwa kutumia miaka mitano madarakani kabla ya kujiuzulu mwaka 2014.

Alirudi kuwa rais tena baada ya kushinda uchaguzi wa mwaka 2018 na kupata muhula wa tatu Desemba 2023, katika uchaguzi ambao wapinzani wake walisema ulikuwa na dosari za ukiukaji wa taratibu.


Kuendelea kwa maandamano hayo kumeungwa mkono na wapinzani, Siteny Randrianasoloniaiko na Rais wa zamani Marc Ravalomanana.

Wawili hao walikataa ofa ya kujiunga na serikali ya Rajoelina, wakisema kufanya hivyo kungekuwa ni “usaliti” kwa wananchi wa Madagascar.

Waandamanaji hawajatoa tamko rasmi la madai, lakini yalianza kama hasira juu ya huduma duni za umma na yamegeuka kuwa wito mpana wa mabadiliko ya kisiasa.

Vijana wengi, wanaokabiliwa na ajira zisizo na uhakika na mishahara midogo, wametaka Rais ajiuzulu, wakimlaumu kwa matatizo wanayopitia.

Wiki hii waandamanaji walionekana wakipeperusha bendera na mabango yaliyoandikwa “Rajoelina ondoka”.

Msemaji wa Gen-Z Mada aliliambia Shirika la Habari la AFP kwamba wanataka Rais ajiuzulu na “kusafishwa kwa Bunge la Kitaifa”.

Wanataka pia Rajoelina awajibike kwa vifo vinavyodaiwa kusababishwa na vikosi vya usalama.

Watumiaji wengine wa mitandao ya kijamii wamekuwa wakitoa wito wa kuvunjwa kwa tume ya uchaguzi na mahakama kuu.

Maandamano hayo yaliyoongozwa na vijana yalisambaa haraka hadi katika miji mingine, yakichochewa na mitandao ya kijamii na maandamano mengine ya “Gen Z” yaliyofanyika katika nchi za Indonesia na Nepal, ambako serikali ziliangushwa.

Madagascar ni miongoni mwa nchi maskini zaidi duniani, ikiwa na kipato cha wastani cha dola 545 kwa mwaka kwa mtu mmoja, kulingana na Benki ya Dunia.

Kisiwa hicho cha Bahari ya Hindi, chenye watu milioni 32, kiliorodheshwa nafasi ya 140 kati ya nchi 180 katika ripoti ya 2024 ya Transparency International kuhusu mtazamo wa ufisadi.


Alikotokea Andry Rajoelina

Ingawa familia yake iliweza kumlipia masomo ya chuo kikuu, Andry Rajoelina aliamua kuacha kuendelea masomo na elimu ya juu ili kuanza kazi kama DJ (Disc Jockey).

Alizaliwa 30 Mei 1974 huko Antsirabe, Madagascar. Ni kati ya watoto watano wa Yves Roger Rajoelina (askari na mkufunzi wa kijeshi) na Olga Rakotomalala Rasoanjanahary.

Andry Rajoelina alipata elimu ya awali Madagascar; kabla ya siasa alikuwa mfanyabiashara, DJ na promota wa mambo mbalimbali ikiwamo muziki.

Alianzisha kampuni ya uchapishaji “Injet” mwaka 1999 na kuchukua kampuni ya matangazo ya familia ya mke wake. Pia alimiliki vituo vya redio na televisheni kama Viva Radio na Viva TV.

Mwaka 2007, alianzisha chama cha siasa kinachoitwa Tanora Malagasy Vonona (TGV Vijana Wamalagasi Walioamua) na kuwania umeya wa Antananarivo.

Alishinda uchaguzi huo wa umeya Desemba 2007 kwa asilimia kubwa ya kura (karibu asilimia 63) na akachukua wadhifa wa Meya wa Antananarivo.

Kwa muda akiwa meya, alikabiliana sana na serikali ya Rais Marc Ravalomanana, akilishutumu kwa ubadhirifu, ukosefu wa uwazi, na jinsi serikali inavyoendeshwa.

Kituo chake cha Viva TV kilifungwa na Serikali mwaka 2008 baada ya kutangaza mahojiano na mwanasiasa aliyewahi kuwa Rais (Didier Ratsiraka).

Uamuazi wa Serikali wa kufungia vyombo vyake vya habari, yaliibuka maandamano kupinga hatua hiyo. Jeshi likaanza kuvuruga nafasi ya Rais Ravalomanana kuendelea madarakani na kuibuka mgogoro wa kisiasa uliopamba moto.

Machi 2009, Ravalomanana alijiuzulu na kuhamisha madaraka kwake kwa jeshi, ambalo baadaye lilimkabidhi Rajoelina uongozi wa Serikali ya Mpito.


Utawala wa Mapito (2009–2014)

Rajoelina aliongoza Serikali ya Mpito tangu alipoingia madarakani kuanzia mwaka 2009 hadi pale uchaguzi ulipoitishwa mwaka 2013.

Machafuko ya kisiasa yalizidi kuendelea ndani ya kipindi hicho, ikinishikizwa na jumuiya za kimataifa na lawama namna alivyopata madaraka.

Alipata kushinikizwa na viongozi wa kimataifa na taasisi za kanda kama Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kumtaka kuboresha mfumo wa uchaguzi.

Imeandaliwa na Noor Shija kwa msaada wa mtandao.