RC Mara: Bodaboda wote kupatiwa mafunzo ya udereva Veta

Butiama. Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi ameiagiza Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) kutoa mafunzo ya udereva na usalama barabarani kwa waendesha bodaboda wote mkoani humo ili kupunguza ajali zinazohusishwa na uendeshaji holela.

Akizungumza jana Ijumaa, Oktoba 3, 2025, katika kikao na wadau wa Butiama FM Radio ikiwa ni maandalizi ya uzinduzi wa kituo hicho, Mtambi alisema ajali nyingi zimekuwa zikisababishwa na waendesha bodaboda wasiokuwa na elimu ya udereva.

“Hapo awali kulikuwa na malalamiko juu ya gharama za mafunzo na leseni ambazo zilikuwa Sh70,000. Tumekubaliana na Veta gharama zishuke hadi Sh30,000. Nitoe wito kwenu wote mkajifunze ili muendeshe kwa usalama na weledi,” amesema.

Amebainisha kuwa bodaboda wana mchango mkubwa katika uchumi wa jamii na taifa kwa ujumla, hivyo si vyema kuendelea kupoteza maisha au kupata ulemavu kwa sababu ya kukosa mafunzo.

“Kuna wakati unakutana na dereva anaendesha pikipiki kwa kasi kana kwamba hataki kurudi nyumbani. Hii kazi ichukulieni kwa uzito wake, ni chanzo cha kipato na huduma muhimu kwa jamii,” amesema.

Kuhusu Butiama FM, Mtambi ameitaka radio hiyo ya jamii kushiriki mapambano ya kimaadili kwa kuelimisha wananchi juu ya changamoto zinazokabili jamii.

“Kuna ukengeufu wa maadili unaoendelea, niiombe radio hii msaidie katika mapambano haya ili jamii yetu ibaki kuwa na maadili mema,” amesema.

Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Butiama FM, Madaraka Nyerere amesema kituo hicho kimeanzishwa kwa lengo la kukuza utamaduni na kutoa jukwaa la wananchi kushiriki katika masuala ya maendeleo.

“Msiseme hii ni radio ya Madaraka, hapana. Ni radio ya jamii nzima. Itakuwa jukwaa la majadiliano baina ya wananchi na Serikali za mitaa katika safari ya maendeleo,” amesema.

Radio hiyo imejengwa katika makazi ya zamani ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, na mchakato wake ulianza mwaka 2012 kabla ya kukamilika kwa gharama ya zaidi ya Sh98 milioni.

Baadhi ya waendesha bodaboda waliounga mkono agizo hilo walisema hatua hiyo imekuja wakati muafaka kutokana na wimbi kubwa la vijana kuingia katika sekta hiyo kwa ajili ya kipato.

Moris Mgendi amesema, “Ajali nyingi zinasababishwa na kutozingatia sheria za usalama barabarani kutokana na kukosa elimu. Hii fursa ya kupata leseni kwa Sh30,000 ni msaada mkubwa, tunamshukuru RC kwa kuliona hili.”

Eliya Wegoro amewaasa wenzake kutumia nafasi hiyo ipasavyo ili kuepuka ajali zinazoweza kuzuilika.