Dar es Salaam. Maendeleo ya sayansi na teknolojia yamebadili mfumo wa maisha ya wananchi, ikiwamo malezi na makuzi ya watoto.
Ni kutokana na hayo, matumizi ya nepi za kitambaa kwa kiasi kikubwa yamepungua, zile za kisasa za kutumia mara moja na kutupa zikichukua nafasi.
Nepi za kuvaa mara moja na kutupa (Diapers) zinatumiwa na wengi pasipo kujali hali ya kipato, kwani huuzwa hata kwa moja kwa gharama ya Sh500.
Hata hivyo, usasa huu umechangia kuharibu mazingira, kwani baadhi ya watu baada ya matumizi huzitupa hovyo, jambo linalosababisha kero mitaani.
Ingawa hakuna takwimu maalumu kuhusu taka zitokanazo na daipa, lakini ni sehemu ya taka ngumu zisizoharibika (zikiwamo plastiki, nyuzi za synthetic na jeli ya kunyonya mkojo) ambazo mifumo ya utupaji wake haiko vizuri.

Wataalamu wa afya na wale wa mazingira wanasema utupaji hovyo wa nepi hizo mbali ya kuchafua mazingira, pia unahatarisha afya ya jamii.
Katika pitapita mitaani, Mwananchi limeshuhudia kwenye baadhi ya maeneo nepi hizo zikiwa zimetupwa kando mwa barabara, kwenye mitaro, mitaani na vichakani.
Saraphina John, mkazi wa Manzese, jijini Dar es Salaam, anasema utupaji holela wa nepi hizo ni kero mitaa inayochangia uchafuzi wa mazingira.
Ali Athumani, mkazi wa Tabata Kinyerezi anasema wakati mwingine diapers (daipa) husambazwa na wanyama kama mbwa au paka wanaozurura mtaani, wakipekua takataka kujitafutia chakula hasa usiku.
“Kama takataka hazijafunikwa na kuhifadhiwa vizuri ni rahisi wanyama kuzifikia na kuzivuruga, hivyo kuchangia taka zikiwemo daipa kuzagaa mitaani,” anasema.
Emmanuel Kamenge, mkazi wa Kimara anasema hali hiyo inaweza kuhatarisha afya hasa ya watoto.
“Watoto wadogo wanaweza kuokota na kuanza kuchezea, jambo ambalo linaweza hatarisha afya zao, ni vyema kuwa makini na kuhakikisha tunazihifadhi vizuri,” anasema.
Magdalena Kalinga, yeye anasema changamoto hiyo huenda inasababishwa na baadhi ya wananchi kutojua namna sahihi ya kuhifadhi aina hiyo ya takataka, hivyo ni vyema elimu itolewe.
Mwenyekiti wa wenyeviti wa mtaa, Wilaya ya Kinondoni, Razalous Anosisye anasema moja ya sababu ya changamoto hiyo ni baadhi ya wananchi kukwepa kulipa fedha ya huduma ya uzoaji wa takataka.
Anosisye anasema matokeo yake baadhi yao huvizia nyakati za usiku wakati watu wamelala, huzitelekeza takataka pembezoni mwa barabara au kwenye mitaro.
“Ninaendelea kusisitiza na kutoa wito kwa wanaofanya haya kuacha mara moja kwani ni kinyume cha sheria na watakapobainika watachukuliwa hatua,” anasema.
Kauli hiyo inaungwa mkono na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Kinyerezi, Hassan Nandeti, anayesema baadhi ya wananchi wasiotimiza wajibu wao wamekuwa sababu ya kuzagaa kwa daipa na aina nyingine za takataka hatarishi.

Anasema hilo linasababishwa na baadhi ya wananchi kuwapa kazi ya kuzoa taka watu ambao hawajawekwa rasmi kwa ajili hiyo.
“Wengine wanawapa watu wa mikokoteni au hata bodaboda na kuwapa fedha kidogo bila ya kuwa na uhakika wa taka hizo wanazitupa wapi, matokeo yake daipa zilizotumika na takataka nyingine kuzagaa hovyo,” anasema.
Amesema pia wapo ambao hawatumii vifaa sahihi vya kuhifadhia takataka.
“Mtu anatumia ndoo iliyopasuka kuhifadhia taka kiasi cha kupitisha uchafu nje na kutofunikwa vizuri, kama uongozi wa mtaa huwa tunatoa elimu juu ya kuzingatia njia sahihi za uhifadhi wa takataka,” anasema.
Vilevile, anaeleza baadhi ya wakandarasi waliopewa jukumu la kuzoa taka hawalitekelezi kwa wakati kulingana na makubaliano, hivyo kufanya taka kuwa nyingi.
Kwa upande wake, mkandarasi wa uzoaji taka wilayani Ubungo, Said Momba anasema changamoto hutokana na baadhi ya wananchi kutotimiza wajibu wao wa kulipa fedha kwa huduma za uzoaji takataka.
Anasema fedha zikilipwa kwa wakati huwasaidia kuendesha shughuli zao vizuri na hata kutoa huduma kwa ufanisi zaidi.
“Changamoto baadhi ya watu sio waelewa, wanaona suala la kulipia huduma ya taka si jukumu lao, wengine hata huzitupa hovyo kwa makusudi, ukiuliza anakuambia siyo kazi yake kuondoa taka alizotupwa sehemu isiyo sahihi,” anasema.
Ameshauri elimu iendelee kutolewa kwa wananchi kuhusu haki na wajibu wao katika suala la utunzaji wa mazingira.
Akizungumza na Mwananchi, Dk Daud Gambo, Meneja mradi wa afya ya mama na mtoto na mtaalamu wa lishe kutoka Shirika la Word Vision, anasema utupaji hovyo wa daipa unasababisha uchafuzi wa mazingira.
Anasema baadhi ya bidhaa hizo kutengenezwa na aina ya malighafi zisizooza kwa haraka, hivyo zikitupa ovyo kuchafua mazingira.
Pia, kutokana na daipa zilizotumika kuwa na kinyesi inaweza kuwa chanzo cha kuzalishwa kwa bakteria na hata kuvutia wadudu wengine ambao ni hatari kwa afya.
“Kinyesi au mikojo iliyomo katika daipa itawavutia wadudu hatarishi kwa afya kama vile nzi kutua na bakteria kuzaliana kwa wingi,” anasema na kuongeza:
“Inakuwa kero kwa wananchi wanaoishi maeneo hayo kwa uchafu na ni uchafuzi wa mazingira, pia si salama kwa afya zao,” anasema.
Daktari bingwa wa mfumo wa upumuaji kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Elisha Osati, anasema hakuna athari za moja kwa moja katika mfumo wa upumuaji, lakini kutokana na daipa hizo zilizotumika kuwa na kinyesi na kuzagaa hovyo, zinaweza kusababisha magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu, homa za matumbo na magonjwa mengine ya aina hiyo.
Hamadi Kissiwa, Meneja wa Usimamizi, Uhamasishaji na Ufuatiliaji wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), amewataka wanaofanya hivyo kuacha mara moja kwani wanasababisha uchafuzi wa mazingira.
Amesema ni kinyume cha Sheria ya Mazingira na kanuni zinazosimamia taka ngumu.
“Kwa sasa hatuna sheria rasmi inayosimamia utupaji wa daipa peke yake, hivyo zinaingia katika kanuni zinazosimamia taka ngumu kwa ujumla wake,” anasema.
Amesisitiza kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha anatunza mazingira, hivyo wabadilike watupe takataka katika maeneo husika na kuachana na dampo bubu.
“Kila mmoja akitimiza wajibu wake kikamilifu basi mazingira yetu yatakuwa safi na salama,” anasema.
Meneja Utekekezaji wa Sheria kutoka NEMC, Amina Kibola ameikumbusha jamii kuwa na utaratibu wa kutenganisha taka, zinazooza na zisizooza, pia kutokana na aina za taka.
Amesema hilo litasaidia kupunguza taka na kutengeneza fursa ya kipato kwa wengine.
Anaeleza taka zinaonekana ni vitu ambavyo havifai kwa matumizi, lakini ni malighafi ambazo zinaweza kutumika kwa maendeleo ya viwanda nchini.
“Ninawaasa wananchi wajue kuwa taka ni fursa lakini ni pale tu zinapotengwa kuanzia pale zinapozalishwa,” anasema.
Amesisitiza kutenga taka kwa usahihi ni muhimu, kwani kila aina ya taka ina namna yake ya uteketezaji.
“Unakuta mtu anataka kuosha vyombo anaenda kumwaga ukoko wa ugali au wali na maji yake ndani ya taka nyingine hii siyo sawa,” anasema.
Katibu Mtendaji wa taasisi inayojishughulisha na masuala ya mazingira ya Agenda for Environment and Responsible Development, Dorah Swai amehimiza elimu kuendelea kutolewa kwa wananchi juu ya namna sahihi ya kuhifadhi taka.
Pia mamlaka zinazohusika na suala la ukusanyaji wa taka na uhifadhi wa mazingira zimetakiwa kuhakikisha zinatekeleza kazi yake kikamilifu.
Njia bora na salama ya kutupa daipa zilizotumika hutegemea mazingira mtumiaji alipo na huduma za uondoshaji taka zilizopo. Inashauriwa kabla ya kuzitupa, kuondoa kwanza kinyesi na kukitupa chooni, hatua inayosaidia kupunguza harufu na uchafuzi wa taka.
Baada ya hilo kufanyika, mtumiaji anapaswa kuifunga kama ambavyo hufungwa wakati wa kumvalisha mtoto au kuiweka kwenye mfuko wa plastiki ili kuzuia harufu na kuvuja.
Kwa maeneo ambayo kuna utaratibu au mfumo wa ubebaji wa taka, unapaswa kuzipeleka eneo la kukusanyia taka za majumbani lililoko kwenye mtaa.
Inashauriwa zisichomwe moto waziwazi kwa kuwa zina plastiki na kemikali ambazo hutoa gesi hatari. Iwapo zinachomwa ni lazima kazi hiyo kufanyika kwenye shimo maalumu la kuchomea taka mbali na nyumba.
Kwa mujibu wa wataalamu zipo nepi za kushonwa kwa pamba au kitambaa maalumu, ambazo hutumika mara nyingi, zikiwa na faida kwani hazina plastiki na ni rafiki kwa mazingira.
Vilevile, ni nafuu kwa kuwa hutumika kwa muda mrefu na hupunguza vipele kwa watoto. Hata hivyo, zinahitaji majisafi na sabuni kuzifua, zikihitaji usafi wa hali ya juu.
Aina nyingine ni zile ambazo nje zina kitambaa unachoweza kukifua, huku ndani ikiwa na tabaka unaloweza kulifua au ukatupa. Hata hivyo, matabaka yanyotupwa hayapaswi kutupwa hovyo.
Kwa mujibu wa wataalamu, zipo pia zinazotengenezwa kwa vifaa vya asili vinavyoweza kuoza kama vile nyuzi za mahindi, mianzi na pamba, ambazo huoza haraka ikilinganishwa na zile zenye plastiki na hazina kemikali nyingi, hivyo ni salama zaidi kwa ngozi ya mtoto. Hata hivyo, inaelezwa bei yake ni kubwa kuliko zile za kawaida.
Wazazi pia wanashauriwa kuwazoesha watoto kujisaidia chooni au kwenye vifaa maalumu mapema ili kupunguza matumizi ya daipa, kwani ni njia ambayo hupunguza gharama, licha ya kuwa inahitaji muda, uvumilivu na uangalizi mkubwa.