Dar es Salaam – Katika hatua isiyotarajiwa, aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Zanzibar, Said Issa Mohammed, pamoja na wenzake Ahmed Rashid Khamis na Maulidah Anna Komu, wamefungua maombi madogo katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala ndogo ya Dar es Salaam, wakidai kuwa Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Tanzania Bara, John Heche, na wenzake wanane wamekiuka maelekezo ya Mahakama yaliyotolewa Juni 10 mwaka huu.
Maombi hayo madogo, yaliyopewa namba 8960 ya mwaka 2025, yanahusiana na kesi ya msingi namba 8323 ya mwaka 2025, inayoendelea kusikilizwa mbele ya Jaji Hamidu Mwanga.
Malalamiko ya Wadai
Kupitia wakili wao, Mulamuzi Patrick Byabusha, walalamikaji wamedai kuwa wadaiwa wameendelea:
Kuitisha na kuandaa mikutano mbalimbali ya ndani ya chama
Kutoa maelekezo ya kazi za kisiasa
Kuzungumza na vyombo vya habari
Hali hii inadaiwa kuwa ni kinyume na marufuku ya Mahakama, iliyopiga marufuku wadaiwa kushiriki shughuli zozote za kisiasa na kiutendaji, kutumia rasilimali za chama au mambo yanayofanana, hadi kesi ya msingi itakapomalizika.
Kesi ya Msingi
Katika kesi ya msingi, wamelalamika kuwa CHADEMA imekuwa:
Kukiitenga Zanzibar katika shughuli mbalimbali za chama, ikiwemo mgawanyo wa mali na rasilimali fedha
Kutumia kauli zinazohusiana na udini na ukosefu wa usawa wa kijinsia
Kufanya vitendo vinavyovuruga muungano wa chama
Walalamikaji wanasema vitendo hivyo vinakiuka Katiba ya CHADEMA, Sheria ya Vyama vya Siasa, na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa sasa, Mahakama inasikiliza maombi madogo haya ili kuamua iwapo maelekezo yaliyotolewa Juni 10 yanaendelea kushikilia mamlaka yao.