Moshi. Wanafunzi wa shule ya sekondari ya Ufundi Moshi (Moshi Technical) mkoani Kilimanjaro, wamebuni njia mbadala ya kukabiliana na uharibifu wa mazingira kwa kutumia taka za plastiki shuleni hapo ikiwemo mifuniko ya chupa, kutengeneza vifaa maalumu vya kupandia maua.
Wanafunzi hao wameonyesha ubunifu huo leo wakati wa mahafali ya 54 ya kidato cha nne yaliyofanyika katika uwanja wa shule hiyo ambapo jumla ya wanafunzi 175 wanatarajia kuhitimu masomo yao mwaka huu.
Akizungumza wakati wa maonyesho hayo, mmoja wa wanafunzi, Gladness Lukumay amesema kuwa wazo hilo lilizaliwa baada ya kuona taka za plastiki zikizagaa katika maeneo ya shule na jirani na wakaamua kuzirejeleza (recycling) kwa kuzitumia kutengeneza bidhaa zenye manufaa.
“Tunakusanya mifuniko ya chupa na taka nyingine za plastiki kutoka sehemu mbalimbali za shule, kisha tunazitengeneza kuwa vifaa vya matumizi kama vile vyombo vya kupandia maua, hii inasaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira,” amesema Gladness.
Aidha, ameongeza kuwa utupaji holela wa taka za plastiki mara nyingi husababisha uchafuzi wa mazingira na huweza kuathiri afya ya jamii kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule hiyo, Philipo Mwanga amesema wanafunzi wa shule hiyo wamekuwa wabunifu wa mambo mbalimbali na kwamba wanajivunia masomo ya amali ambayo kwa kiasi kikubwa yameleta mabadiliko chanya katika shule hiyo.
“Amali imekuwa msaada mkubwa sana kwa wanafunzi wetu hasa wenye mahitaji maalumu kwa sababu ni vitendo zaidi, matumizi ya ubao ni asilimia ndogo sana wanashinda kufanya vitu kwa vitendo,” amesema Mwalimu Mwanga.
Amesema: “katika mahafali haya tumeona vitu vingi wametengeneza, kubadilisha ngozi kuwa vifaa mbalimbali, mbao kuwa vifaa pamoja na plastiki kuwa vifaa mbalimbali kwenye shule hii hakuna sehemu yoyote kuna chuma chakavu maana zinaokotwa kama vitendea kazi, mbao hutaona zikizagaa wanapita na kutengeneza vitu mbalimbali.”
Amesema kwa sasa wanafunzi wa shule hiyo wanatengeneza viatu, mikanda, pochi, skafu za skauti. “Tunakoelekea sasa tutakuwa na kiwanda kamili kwa sababu tuna ukaribu mkubwa na kiwanda cha ngozi cha Kilimanjaro (KLICL).
Aidha, ameishukuru serikali kwa kuwapatia fedha na kuweza kununua mashine mbili ambazo tayari zinatumiwa na wanafunzi shuleni hapo.
Akizungumza katika mahafali hayo, mmoja wa wadau wa elimu, Shaban Mwanga amesema kwa ubunifu huo ambao wanafunzi wameonyesha ni dhahiri kwamba wanahitaji kutafutiwa kiwanda kidogo kwa ajili ya uzalishaji wa bidhaa mbalimbali.
“Tumeona wanafunzi wana uwezo wa kushona, kutengeneza viatu, mikoba pamoja na vifaa vingine hivyo kuna haja ya kuishauri shule kutafuta wadau ambao wanaweza kufungua kiwanda kidogo ndani ya shule hii wakishirikiana na viwanda vingine, wanafunzi wanaweza kunufaika na wazazi pia nao wanaweza kunufaika,” amesema mdau huyo wa elimu.
Amesema: “Mimi kama mdau wa maendeleo, nimewiwa kuzungumza na walimu tuje kukaa pamoja, lakini tutaendelea kuiambia serikali kilichopo hapa shule ya sekondari ya Moshi Technical, sisi tupo tayari kuiunga serikali mkono.”