Arusha. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, imemuhukumu Cosmas Msumari adhabu ya kunyongwa hadi kufa baada ya kukutwa na hatia ya kumuua kaka yake, Lucas Msumari, kwa kumpiga na nyundo kichwani.
Tukio hilo lilitokea Aprili 6,2023 katika mtaa wa Togo, wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam, ambapo ndugu hao wawili walikuwa wakiishi katika chumba kimoja kama wapangaji na kufanya kazi ofisi moja katika idara tofauti.
Hukumu hiyo imetolewa Septemba 30,2025 na Jaji David Ngunyale aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa mahakama.
Jaji baada ya kupitia ushahidi wa pande zote mbili, Jaji Ngunyale alieleza kuwa Mahakama imemkuta Cosmas na hatia ya mauaji na kumuhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.
Miongoni mwa ushahidi uliotumika kumtia hatiani ni pamoja na maelezo ya onyo ya mshtakiwa ambaye alikiri kuhusika na mauaji hayo, ambapo pia alienda kuonyesha polisi mahali alipokuwa ameficha nyundo aliyoitumia kwa mauaji hayo pamoja na duka aliloinunua.
Cosmas alishtakiwa kwa kosa la mauaji kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu.
Ilielezwa mahakamani hapo kuwa siku ya tukio Lucas (marehemu kwa sasa), hakufika kazini wala simu yake haikupokelewa ambapo wafanyakazi wenzake walitoa taarifa kwa shahidi wa kwanza wa Jamhuri, Lucia Msumari (dada yao).
Shahidi huyo alimpigia simu shahidi wa pili na kumwelekeza aende walipokuwa wakiishi ndugu zake ili kuuliza nini kinaendelea.
Shahidi wa pili alidai alipofika eneo hilo alikuta habari mbaya kuhusu kifo cha Lucas, ambapo alishindwa kumweleza shahidi wa kwanza (dada wa marehemu na mshtakiwa).
Ilidaiwa mahakamani hapo Lucia alilazimika kuacha shughuli zake na kuelekea huko na alipoikaribia nyumba hiyo aliona watu wakiwa wamekusanyika na alipoingia ndani ya chumba alimkuta kaka yake akiwa amefariki, huku akivuja damu.
Lucia alieleza mahakamani kuwa marehemu alikuwa na akikaa na mshtakiwa lakini baada ya tukio hilo Cosmas hakuonekana hadi maziko yakafanyika kisha akakamatwa baadaye na Polisi.
Mshtakiwa alikamatwa na shahidi wa nne, D 9688 Haji Ramadhan, Aprili 9,2023 akihusishwa na mauaji hayo ambapo alihojiwa na shahidi wa saba Sajenti Amiri.
Shahidi huyo alisema kuwa wakati wa kuandika maelezo ya onyo, mshtakiwa alikiri kumuua kaka yake na kudai kuwa alikuwa mtukutu ambapo alienda pia kuonyesha mahali alipoficha nyundo aliyokuwa ameitumia kwa mauaji hayo.
Shahidi wa tano, F 4793 alisema, Aprili 10,2023 akiwa na shahidi wa kujitegemea, (shahidi wa sita), Ludovick Karugaba, walionyesha ilipokuwa imefichwa nyundo hiyo.
Ilieleza mahakamani hapo kuwa Aprili 12,2023 mshtakiwa aliwapeleka polisi mahali alipokuwa amenunua nyundo hiyo, katika duka la shahidi wa nane anayeuza vifaa vya ujenzi ambaye alimkumbuka mshtakiwa kuwa alinunua nyundo hiyo kwa bei ya Sh14,000.
Shahidi wa 13, Profesa Amos Makigonja, aliufanyia uchunguzi mwili wa Lucas, (marehemu) na kuthibitisha kuwa chanzo cha kifo hicho kilikuwa jeraha kubwa la kichwani.
Katika utetezi wake, Cosmas alikana kosa hilo na kueleza kuwa alikuwa akifanya kazi ya kufanya usafi na utunzaji wa nyumba kwa mtu ambaye alikuwa akimlipa Sh40,000.
Alisema kuwa alikuwa akiishi kwenye nyumba ya mwajiri wake ambapo hakuwa na mawasiliano ya mara kwa mara na ndugu zake, na siku ya tukio hilo alikuwa nyumbani kwa mwajiri wake na hakuwa akiishi na Lucas kama ilivyodaiwa.
Alieleza mahakamani hapo kuwa walimletea nyundo ambayo hakuijua na akalazimika kusaini taarifa asiyoijua na kupelekwa kwa mwanamke aliyedaiwa kumuuzia nyundo.
Baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili, Jaji alisema mahakama itaangalia iwapo upande wa mashtaka umethibitisha kesi hiyo pasipo kuacha shaka.
Alisema upande wa mashtaka unapaswa kuthibitisha vipengele vya kosa na viambato vya kosa la mauaji vinavyopatikana kutokana na kifungu kilichoanzisha kosa hilo, cha 196 cha Kanuni ya Adhabu ambapo inapaswa kuthibitishwa marehemu alikufa kifo ambacho hakikuwa cha asili, iwapo mshtakiwa alihusika na mauaji hayo na alikuwa na nia mbaya.
Alisema kwa uchunguzi wake kutokana na ushahidi uliotolewa, kifo cha Lucas hakikuwa cha asili, ushahidi uliothibitishwa na shahidi wa 13,aliyeufanyia uchunguzi mwili huo ambaye alibaini jeraha kubwa kichwani kwa marehemu.
Jaji alisema kuhusu iwapo mshtakiwa alihusika na mauaji hayo, hakuna shahidi aliyeshuhudia mshtakiwa akitenda kosa hilo na kuwa katika kujibu suala hilo, mahakama itazingatia ushahidi wa kimazingira.
Jaji alisema ushahidi wa shahidi wa kwanza uko wazi kuwa mshtakiwa na Lucas (marehemu kwa sasa) ni ndugu zake wa damu waliozaliwa na Katarina Cosmas na Cosmas Msumari na kuwa ndugu zake walikuwa wakiishi chumba kimoja mtaa wa Togo.
Jaji alisema ushahidi kuwa marehemu alikuwa akiishi na mshtakiwa chumba kimoja ulithibitishwa na shahidi wa pili, tatu na shahidi wa tisa ambaye alikuwa mpangaji mwenzao katika nyumba hiyo.
Jaji alisema ushahidi wa upande wa mashtaka umethibitisha kuwa mshtakiwa alikuwa akiishi na kaka yake hadi siku ya kifo ambapo marehemu aliuawa akiwa amelala kitandani.
Baada ya kuchambua ushahidi wa pande zote, Jaji alisema upande wa mashtaka umethibitisha kosa kuwa mshtakiwa ndiye alimuua kaka yake kwa sababu walikuwa wakiishi pamoja, ndiye aliyenunua nyundo aliyoitumia kutenda kosa hilo.
“Jambo hilo limethibitishwa pasipo shaka yoyote kwamba mshtakiwa alikuwa na maandalizi ya kutenda kosa hilo kwa kununua nyundo na alikuwa eneo la uhalifu ambapo kosa hilo lilitendeka. Kutokana na ushahidi uliopo kwenye kumbukumbu, sina shaka kwamba mtuhumiwa alitenda kosa aliloshtakiwa nalo,”
Jaji alifafanua kuwa kukiri kwa mshtakiwa kunapelekea kugundulika ni wapi alikuwa ameficha nyundo na alinunua wapi na kukiri katika kesi hiyo ni ushahidi mzuri wa kumtia hatiani.
Alisema mshtakiwa amekiri makosa yake kwa kueleza vipengele vyote vya kosa.
“Nimeridhika kwamba upande wa mashtaka umethibitisha kosa linalomkabili mshtakiwa bila ya shaka yoyote, kama inavyotakiwa kisheria. Kwa hivyo, mshtakiwa anatiwa hatiani kwa mauaji Kinyume na Kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu,” alihitimisha Jaji kwa kusema kuwa kutokana na hilo anamuhukumu kunyongwa hadi kufa.