Ayoub aahidi kuondoa changamoto ya maji Chaani

Unguja. Mgombea ubunge Chaani, Ayoub Mohamed Mahmoud ameahidi kuchimba visima vinane na kuweka matanki manne ya maji ili kumaliza usumbufu wa upatikanaji majisafi na salama jimboni humo.

Hayo ameyasema leo Jumapili Oktoba 5, 2025 katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Chaani, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Amesema, jimbo hilo linakabiliwa na changamoto ya majisafi na salama hivyo atahakikisha analipatia ufumbuzi suala hilo, iwapo atapewa ridhaa ya kuliongoza.

“Tumeligawa jimbo zoni nne kwa lengo kuchimba visima vinane na matanki manne ya maji kila wadi kwa lengo la kuondoa changamoto ya maji,” amesema Ayoub.

Mbali na hilo, Ayoub amesema atawekeza kuwapa elimu bora wanafunzi kwa  kuhakikisha wanaendana na kasi ya mabadiliko ili kuingia na kushinda ushindani wa soko la ajira.

Pia amesema, atahimiza amani na utulivu, “ili amani ipatikane lazima wananchi wawe na umoja na mshikamano kwa lengo la kukiwakilisha chama hicho.”

Pia ameahidi kuweka asasi mahususi ya kuwatumikia wakulima kuzalisha chakula kwa wingi na kwa kuwa jimbo hilo linategemea zaidi kilimo   atawatengenezea mazingira kwa kuwapa matrekta ya kulimia.

Mbali na hilo, amesema kiwango cha ufaulu jimboni humo kipo chini, hivyo atahakikisha  wanafunzi wote wanaokaa kambi ili kupata muda mwingi wa kusoma.

Amesema, ataweka fungu maalumu la kuwasaidia wanafunzi ambao hawana uwezo wa kusomeshwa na wazazi kutokana na hali duni za maisha.

Naye, mgombea uwakilishi Chaani, Juma Usonge Hamad amesema ataacha alama katika utendaji wa awamu hii kwa kuunganisha nguvu zao za pamoja kuleta maendeleo.

Amesema, atawatumika wananchi wa jimbo hilo bila ya ubaguzi wowote kwa sababu ameshakuwa mtumishi wa wananchi hivyo na hatosita kuwatumikia.

Naye, mgombea udiwani Chaani, Khamis Haji amesema yupo kwa ajili ya kutumwa na wananchi wa jimbo hilo kwa sababu ya kutafuta chaani mpya yenye maendeleo kwa kila mmoja.

Amesema endapo wananchi wakimchagua atashuka chini kutafuta changamoto zao na kuzitatua.