Bodi ya Ligi Kuu Bara imewatangaza washindi wa mwezi Septemba kwenye ligi hiyo kwa upande wa kocha na mchezaji.
Golikipa wa Yanga Djigui Diarra na Kocha wa JKT Tanzania ndio mastaa wa mwezi Septemba wa Ligi Kuu Bara.
Katika taarifa iliyotolewa na bodi hiyo imesema:
“GOLIKIPA wa timu ya Young Africans, Djigui Diarra amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Septemba wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa mwaka 2025/2026, huku Ahmad Ali wa JKT Tanzania, akichaguliwa kuwa Kocha Bora wa ligi hiyo kwa mwezi huo”.
“Diarra alionesha kiwango kizuri chenye mwendelezo akiwashinda Anthony Tra Bi wa Singida Black Stars na Mohamed Bakari wa JKT Tanzania alioingia nao fainali katika mchakato wa Tuzo za Mwezi uliofanywa na Kamati ya Tuzo za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)”.
“Mchezaji huyo alitoa mchango mkubwa kwa timu yake katika michezo miwili ambayo Young Africans ilicheza na kupata ushindi kwa mchezo mmoja dhidi ya Pamba Jiji (3-0) na kupata suluhu ya (0-0) dhidi ya Mbeya City hivyo kutokuruhusu goli kufungwa kwa timu yake”.
“Kwa upande wa Ahmad Ali aliyeingia fainali na Romain Folz wa Young Africans na Miguel Gamondi wa Singida Black Stars, aliiongoza JKT Tanzania kwenye kiwango kizuri katika michezo miwili iliyocheza kwa mwezi huo wa Septemba”.
“JKT Tanzania ilipata sare ya bao moja dhidi ya Mashujaa wakiwa ugenini, uwanja wa Lake Tanganyika Kigoma na kupata ushindi wa mabao mawili dhidi ya Coastal Union (1-2) wakiwa kwenye uwanja wa ugenini, Mkwakwani Tanga”
Hizi ni tuzo za kwanza za mwezi msimu wa 2025/26 ikiwa tayari zimechezwa mechi 19 katika mwezi Septemba.