KAMA kuna taarifa ambayo mashabiki wengi wa Yanga wanaisubiri ni hatma ya kocha wa timu hiyo, Romain Folz.
Si unakumbuka kocha huyo aliwagawa viongozi kutokana na presha iliyopo kutoka kwa mashabiki ambao hawamuelewi, sasa inaelezwa ana takribani saa 24 ili kujua kama ataendelea kuwepo au la kutegemea na uamuzi wa kigogo mmoja aliyeshikilia faili lake kwa sasa.
Kocha huyo raia wa Ufaransa amekuwa katika presha kutoka kwa mashabiki wanaoshinikiza apigwe chini kutokana na kushindwa kumwelewa kwa jinsi timu inavyocheza bila kuwapa burudani waliyoizoea kupitia makocha waliomtangulia.
Ipo hivi. Mashabiki wa Yanga hawaielewi timu hiyo inashinda, lakini hawana furaha na namna ushindi unavyopatikana wakiona kama soka inalocheza haliwavutii japo kocha huyo hajapoteza mechi yoyote kati ya 10 ilizocheza timu hiyo zikiwamo tano za kimashindano na tano za kirafiki.

Presha hiyo ya mashabiki imewaingia mabosi wa klabu hiyo, lakini kuna mtu mmoja tu ambaye ndiye anasubiriwa kumaliza jambo hilo ambaye ni Rais wa klabu hiyo, Injinia Hersi Said.
Hersi ndiye aliyeshikilia batani ya ajira ya Folz na taarifa za ndani zinasema bosi huyo kwa siri sana ameshaanza kupitia CV za makocha wakubwa akijiandaa na jambo lolote hasa baada ya kikao kizito kinachotarajiwa kufanyika kesho Jumanne ikiwa ni saa 24 zijazo ili kuamua hatma ya Mfaransa huyo.
Inadaiwa kuwa, mabosi wengine wa Yanga wanamsubiria Injinia Hersi kutegua kitendawili hicho na atakaporejea nchini akitokea DR Congo alikokwenda kushiriki Mkutano wa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) wakati wowote kuanzia kesho Jumanne kunaweza kutolewa msimamo mzito.

Hersi bado hajaonyesha ni uamuzi gani atachukua kumbakisha kocha huyo au kumsitishia mkataba akiendelea kuusoma mchezo, licha ya presha hiyo ya mashabiki iliyokolezwa zaidi baada ya suluhu dhidi ya Mbeya City katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
“Unajua rais tu (Hersi) ndiye mwenye uamuzi ya mwisho, wapo ambao wameongea naye ambao hawakubaliani na kocha anawaelewa, lakini wapo wanaokubaliana na kocha amewasikiliza na amekubaliana nao sasa uamuzi gani atachukua hapo ndio hatujafahamu,” amesema mmoja wa vigogo wa klabu hiyo.
“Tunamsubiri arudi huko DR Congo ndipo tutajua uamuzi gani utachukuliwa kama ataondoka au vinginevyo jambo linalochanganya ni tunaambiwa rais ameshaanza kusaka kocha taratibu.”
Wakati presha ikiwa hivyo. Folz mwenyewe alikuwa arejee nchini jana Jumapili kutoka Afrika Kusini alikokwenda kwa mapumziko ya muda mfupi.

Folz alijipa mapumziko na kutoa pia kwa timu nzima kwa muda wa siku tatu ambapo leo wanatarajia kurudi kazini kuendelea maandalizi ya mechi zijazo za raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Ligi Kuu. Yanga imepangwa kuvaana na Silver Strikers ya Malawi kati ya Oktoba 17-26 kusaka tiketi ya kwenda makundi kwa mara ya tatu mfululizo baada ya kucheza hatua hiyo misimu miwili iliyopita.
“Kocha anatarajiwa kurejea leo (jana) Jumapili kwani alitoa mapumziko ya siku tatu kwa timu nzima kabla ya kukutana kesho (leo) Jumatatu,” kimesema chanzo kutoka Yanga.