Katibu Bavicha adaiwa kuchukuliwa na watu wasiojulikana

Njombe. Katibu wa Baraza la Vijana jimbo la Lupembe, Abedinego Sanga, anadaiwa kuchukuliwa na watu wasiojulikana akiwa katika eneo analofanyia biashara zake huko Matembwe, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe.

Hayo yamesemwa leo Jumapili Oktoba 5, 2025 na Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Njombe, Seth Vegula.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga amesema wamepokea taarifa za tukio hilo baada ya kupigiwa simu usiku.

“Nilipata taarifa baada ya kupigiwa simu kutoka eneo la tukio na inasemekana  limetokea jana saa moja na nusu kuelekea saa mbili usiku.”

“Kwa sasa askari wapo hapo Lupembe na kuna wananchi wanatoa maelezo na baada ya hapo, tutaanza uchunguzi wa jambo hilo na kubaini hilo gari na chanzo ni nini ila siwezi kusema kama ni mtu wa Bavicha ametekwa, ila kuna mtu amekamatwa na watu ambao hawajafahamika” amesema Kamanda Banga.

Mwenyekiti Vegula amedai kwamba taarifa walizopokea kutoka Matembwe zinaeleza kuwa Sanga anadaiwa kuchukuliwa na vijana wasiojulikana saa 1:30 usiku na kuingizwa kwenye gari aina ya Toyota Landcruiser lenye rangi nyeupe ambalo halikuwa na namba.

“Tumeambiwa gari hilo lilisimama mlangoni mwa duka lake la dawa. Kwa mujibu wa maelezo ya mashuhuda ni kwamba, alishuka mtu mmoja kutoka kwenye gari hilo na kuingia dukani kisha kumwambia Abedinego anahitajika kwenye gari, lakini alikataa na kumuuliza kuna kitu gani,” amedai Vegula.

Amedai baada Sanga kukataa, alishuka mtu mwingine kutoka kwenye gari hilo na kutaka kumshika kwa lazima ndipo alianza kupiga kelele kuwa anatekwa na majirani wakaanza kusogelea eneo hilo.

“Majirani walipoanza kusogea ndipo wakashuka watu wengine wawili wenye silaha na kuwatisha wananchi kuwa wakisogea watawapiga risasi kwa sababu Sanga anahusika na mauaji ya mwanafunzi, ndiyo maelezo ya watu hao,” amesimulia Vegula.

Amesema pamoja na kujitambulisha kuwa wao ni askari polisi, lakini hawakueleza kwa kina huyo Katibu anahusika na mauaji ya mwanafunzi yupi na wapi, matokeo yake waliendelea kuwatisha wananchi na hatimaye kuondoka naye.

Amesema watu hao pia walichukua simu ya Sanga na kuanza kutuma ujumbe mfupi wa maandishi kwa watu wa karibu kupitia namba zilizopo kwenye simu yake kuanzia saa tatu kuelekea saa nne usiku.

Amesema jitihada za kumtafuta  zinaendelea na wameshatoa taarifa kituo cha polisi Lupembe.

“Katibu wa Chadema wilaya ya Njombe amewasiliana na Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Njombe   lakini akadai hana taarifa na hajui chochote,” amesema kiongozi huyo.

Katibu wa Chadema Jimbo la Lupembe, Emmanuel Uhagile ameliomba Jeshi la Polisi kufuatilia tukio hilo ili kuwakamata wanaohusika.

“Mazingira ya ndani pale walimpiga na damu zinaonekana na mke wake mpaka sasa anafuatilia polisi na kwa mujibu wao wapelelezi kutoka Njombe watakuja,” amesema Uhagile.