KINDA wa Tanzania anayekipiga Trident FC ya Zambia, Mourice Sichone amesema maumivu ya kidole cha mguu aliyopata mazoezini yatamweka nje ya uwanja kwa takribani wiki tatu.
Kinda huyo (18) alisajiliwa dirisha dogo akitokea Mpulungu Harbour FC ya nchini humo akicheza mechi 12 na kufunga mabao manne na asisti tano.
Akizungumza na Mwanaspoti, Sichone amesema aliumia mazoezini na ripoti ya daktari inaonyesha atakaa nje kwa wiki tatu hadi atakapokuwa sawa.
Aliongeza ingawa siyo jeraha kubwa lakini amekuwa akipata shida kwenye kupiga mpira akipitia maumivu makali na hadi sasa amekosa takribani mechi nne za ligi.
“Nimebakiza wiki moja kukamilisha ratiba ya matibabu na wiki ijayo nitaanza mazoezi madogo madogo naamini nitakuwa sawa maana nimejitonesha mara mbili eneo hilo,” amesema Sichone.
Tangu ligi Daraja la Kwanza Zambia ianze kuchezwa msimu huu zimepigwa mechi tano na kinda huyo wa zamani wa Azam FC ya Vijana U-20 alicheza mechi moja.