Kocha wa timu ya Pamba Jiji, Francis Baraza ametoa pongezi kwa usajili ilioufanyika Stand United, huku akikiri kazi uwanjani umeonekana kupitia wachezaji hao.
Akizungumza baada ya mechi ya kirafiki iliyozikutanisha timu hizo Oktoba 04, 2025 kwenye Uwanja wa CCM Kambarage mkoani hapa na kumalizika kwa matokeo ya 0-0, ameeleza usajili uliofanywa na Stand United unaashiria timu hiyo itapanda ligi kuu.
“Naona Stand wamesajili wachezaji wazuri wenye uzoefu katika mchezo, kazi yao tumeiona uwanjani wanafanya vizuri, pia timu yangu ya Pamba tuko vizuri japo tulikuwa na majeruhi lakini muda wa mapumziko umetusaidia kurudi katika hali nzuri,” amesema Baraza.
Kwa upande wake Kocha wa Stand United, Iddy Cheche ameeleza kuwa kuna upungufu ameuona kutokana na mechi hiyo ya kirafiki na wanakwenda kufanyia kazi.
“Kwa muda uliobaki unatosha kabisa kufanya marekebisho kwa mapungufu tulioyaona uwanjani lakini sio makubwa, muda uliobaki kucheza Championship unatosha kufanya marekebisho,” amesema Cheche.
Aidha, Msemaji wa Stand United, Ramadhan Zoro ametambulisha kikosi cha timu hiyo kikiwa na wachezaji wapya kutoka timu mbalimbali za nchini Tanzania akiwemo Feruz Teru aliyekuwa mlinda mlango wa timu ya Simba.