Lamine azipiga mkwara Simba, Yanga

NYOTA mpya wa Singida Black Stars, Lamine Diadhiou Jarjou amesema anaona ni heshima kubwa kwake na wenzake kuwa sehemu ya mafanikio ya timu hiyo, huku akizipiga mkwara Simba, Yanga na Azam FC katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Jarjou amesema hayo, jana Jumamosi alipozungumza na Mwanaspoti katika paredi la timu hiyo baada ya kurejea Singida BS ikiwa na ubingwa wa Kombe la Kagame 2025 ambayo timu hiyo ilitwaa mwezi uliopita ikiitambia Al Hilal ya Sudan.

Winga huyo aliyejiunga na Singida BS akitokea Ufaransa alikokuwa akiichezea Grenoble Foot 38 ya Ligue 2, amesema kila mmoja katika kikosi hicho ana furaha kubwa kwa hatua iliyofikiwa na klabu hiyo.

“Ni mafanikio makubwa kwa klabu na wachezaji, naamini kila mtu yupo na furaha. Ukiangalia kiwango cha ushindani Afrika Mashariki, kuna klabu kubwa sana (Simba, Yanga na Azam) na sisi tupo hapa kushindana nao,” amesema Jarjou.


Singida BS ipo nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Bara nyuma ya Simba kila moja ikiwa na  pointi sita, zikitofautiana uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa, pia ikiwa imetinga raundi ya pili katika Kombe la Shirikisho Afrika ikiing’oa Rayon Sports ya Rwanda kwa ushindi wa mabao 3-1.

Jarjou, ambaye ni raia wa Gambia, alieleza sababu ya kujiunga na Singida Black Stars ni sehemu ya mpango ambao alikuwa nao wa kurejea nyumbani barani Afrika.

“Tanzania ipo Afrika, kwa hiyo mimi nimeamua kurudi nyumbani. Walionikaribisha walikuwa wengi, siwezi kumtaja mtu mmoja,” amesema.

Kuhusu matarajio yake na timu hiyo, amesema; “Sababu ya kuja hapa ni kupambana. Hatujaja tu kushiriki, tumekuja kupigania ubingwa.”

Jarjou alifichua pia kuwa si mara yake ya kwanza kuwepo Tanzania, kwani mwaka 2023 aliwahi kuja na timu yake ya zamani ya Al Hilal kutoka Sudan.

Kwa mashabiki wa Singida Black Stars, Jarjou aliomba waendelee kutoa sapoti kwa kikosi hicho.