Lipumba ataja ujenzi wa demokrasia akionya vyombo vya ulinzi kuingilia siasa

Dar es Salaam.  Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba amesema Tanzania inahitaji ujenzi wa demokrasia ya kweli huku akitoa wito kwa vyombo vya ulinzi na usalama kuacha kuingilia masuala ya siasa.

Akizungumza hayo katika mkutano wa kampeni uliofanyika leo Octoba 5,2025 kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Mbagala Rangi Tatu, kata ya Kibonde Maji, Profesa Lipumba amesema chama hicho kinashiriki katika uchaguzi kwa sababu ya uzalendo na nia ya kuona nchi inapata maendeleo ya kisiasa.

Amesisitiza kura zihesabiwe kama zitakavyopigwa na wananchi na wakataoshinda watangazwe na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kwenda kupiga kura Jumatano Oktoba 29, 2025.




“Kura zikipigwa zitangazwe kama zilivyopigwa, kusiwe kama uchaguzi wa 2020, tuwe na uchaguzi utakaokuwa bora kuliko wa 2015 watu wakapige kura na zihesabiwe kama zitakavyopigwa kwa haki,” amesema Profesa Lipumba.

Amesisitiza kuwa ni muhimu kwa vyombo vya dola kuepuka kuingilia shughuli za kisiasa, akiongeza kuwa uchaguzi unapaswa kuwa huru na haki.

Akizungumza katika mkutano huo, Mgombea ubunge wa chama hicho Jimbo la Mbagala, Sheikh Said Kinyogoli amewaahidi wananchi wa jimbo hilo kuwa atahakikisha anatatua changamoto ya mikopo inayowaumiza wajasiriamali wadogo na vikundi vya wanawake.

Kinyogoli amesema atajitahidi kuanzisha Saccos ya jimbo ili kuondoa mikopo ya asilimia kumi inayowatesa wanawake aliyosema imeshindwa kutatua changamoto zao za kimaisha.

“Najua mmetapeliwa na serikali zilizopita kwa kutoa hela kidogo ili mpate mikopo kidogo ambayo haijatusaidia na wengine hawakupata kabisa,” amesema Kinyogoli.

Ameongeza kwamba atashughulikia pia changamoto ya michango ya mara kwa mara kwa shule, akisisitiza kuwa elimu inapaswa kuwa bure kwa kila Mtanzania.