Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WiLDAF Tanzania) kwa kushirikiana na serikali na wadau wengine wa maendeleo, limeandaa Mdahalo wa Kitaifa unaolenga kujadili changamoto za ukatili unaotumia teknolojia na ukatili dhidi ya wanawake katika siasa na uchaguzi.
Mdahalo huo umefanyika Oktoba 3, 2025 jijini Dar es Salaam na umehudhuriwa na wawakilishi wa serikali, mashirika ya Umoja wa Mataifa, wanaharakati wa haki za wanawake, wanasheria, vyombo vya habari na asasi za kiraia, wote wakijadili mikakati ya kulinda usalama wa wanawake katika majukwaa ya siasa, hususan kipindi kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025.
Akifungua mdahalo huo, Mkurugenzi wa WiLDAF Tanzania, Wakili Anna Kulaya, alisisitiza kuwa ukatili unaochochewa na teknolojia ni tishio jipya kwa demokrasia, hasa unapolenga wanawake viongozi, wagombea na wanaharakati wa kisiasa.
“Kukomesha ukatili dhidi ya wanawake kwenye siasa na uchaguzi si suala la wanawake pekee; ni suala la kuimarisha demokrasia na kulinda utu wa kila raia,” alisema Bi. Kulaya.
Aliongeza kuwa mdahalo huo ni sehemu ya maandalizi ya kampeni ya Siku 16 za Uanaharakati Dhidi ya Ukatili wa Kijinsia, ambapo mwaka huu kauli mbiu kuu ni “Linda Jamii, Komesha Ukatili wa Kidigitali na wa Kijinsia.”
Bi. Kulaya alitumia nafasi hiyo kuwashukuru wadau wa maendeleo waliounga mkono mdahalo huo, wakiwepo UN Women, GIZ, UNDP, UNFPA na Ubalozi wa Ireland, Uswizi, na Ubelgiji kwa kuendelea kushirikiana na WiLDAF katika juhudi za kuimarisha haki za wanawake.
Akitoa hotuba kwa niaba ya serikali, Mwakilishi wa Wizara ya Katiba na Sheria alisema kuwa ukuaji wa teknolojia umechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza uwazi na upatikanaji wa habari, lakini pia umeleta changamoto za ukatili wa kidigitali, hususan dhidi ya wanawake.
“Vitendo kama lugha za chuki, usambazaji wa taarifa za uongo, na unyanyasaji mitandaoni vinaharibu hadhi ya wanawake na kuvunja misingi ya usawa,” alisisitiza mwakilishi huyo.
Aliongeza kuwa serikali imeshapitisha sheria tatu muhimu mwaka 2024, ikiwemo Sheria ya Uchaguzi, ambayo katika Kifungu cha 135 inakataza ukatili wa kijinsia na unyanyasaji dhidi ya wagombea wanawake.
“Tunataka wanawake washiriki siasa bila hofu. Tunataka uchaguzi wa amani, usawa na heshima,” aliongeza.
Katika mjadala huo, Sisty L. Nyahoza, Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, alisisitiza umuhimu wa vyama vya siasa kuwa mstari wa mbele katika mapambano haya kwa kuhakikisha sera na katiba zao zinapinga aina zote za ukatili wa kijinsia.
“Mwaka jana (2024) Sheria ya Vyama vya Siasa ilirekebishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kukitaka kila chama cha siasa kiwe na sera ya jinsia pamoja na dawati la jinsia ili kudhibiti ukatili wa kijinsia ndani ya vyama vya siasa na katika siasa,” alisema Nyahoza.
Aidha, alionya kuwa vitendo vya udhalilishaji kupitia mitandao ya kijamii vinaendelea kuwakatisha tamaa wanawake wengi wenye ndoto za kugombea au kushiriki kwenye siasa.
“Watu wanaweka kwenye mitandao ya kijamii ujumbe, picha na maneno ya hovyo ya kudhalilisha wanawake ili kuwaogopesha wasishiriki katika siasa. Haya ni mambo yanayopaswa kupigwa vita kwa pamoja,” aliongeza.
Mdahalo huu umebeba ujumbe mzito wa kuhimiza ulinzi wa haki za wanawake na ushiriki wao salama katika siasa, kwa kutambua kuwa pale ambapo wanawake wananyamazishwa, demokrasia inadorora.
“Tukilinda heshima ya wanawake wanaoongoza leo, tunalinda demokrasia ya kesho,” ulisisitiza ujumbe wa WiLDAF.
Mdahalo huu umefungua ukurasa mpya wa mjadala wa kitaifa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025, ukiwa ni jukwaa la kujenga mikakati ya pamoja dhidi ya ukatili wa kidigitali na wa kijinsia, na kuchochea Tanzania yenye uchaguzi wa amani, ushirikishwaji na usawa kwa wote.

