MENEJA WA TRA DODOMA AONGOZA BONANZA LA MICHEZO KWA WATUMISHI

 

 

Dodoma

Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Dodoma, Bw. Pendolake Elinisafi, ameongoza watumishi wa mamlaka hiyo kushiriki katika bonanza maalum la michezo lililolenga kujenga na kuimarisha afya pamoja na kuongeza mshikamano miongoni mwao.

Bonanza hilo lililofanyika katika viwanja vya Kilimani Park jijini Dodoma, limehudhuriwa na watumishi kutoka vitengo mbalimbali vya TRA na lilipambwa na michezo ya kuvutia ikiwemo mpira wa miguu, kuvuta kamba, mbio za magunia, kukimbiza kuku, kutembea na yai kwenye kijiko, na mpira wa pete.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa bonanza hilo, Bw. Elinisafi alisisitiza umuhimu wa michezo katika kujenga afya bora na kuimarisha mahusiano kazini. “Michezo ni njia mojawapo ya kuimarisha afya ya mwili na akili, lakini pia huchangia katika kujenga mshikamano na ari ya kufanya kazi kwa pamoja kama timu,” alisema.

Watumishi walionekana kufurahia michezo hiyo ambayo iliibua ushindani wa kirafiki na kuongeza furaha, huku ikidhihirisha umuhimu wa matukio ya kijamii kazini. Washiriki walitunukiwa zawadi mbalimbali kama sehemu ya kutambua ushiriki wao na kuwahamasisha kuendelea na utamaduni wa kushiriki michezo kazini.

Bonanza hilo limeonesha kuwa, mbali na majukumu ya kikazi, TRA inatambua umuhimu wa shughuli za kijamii na kiafya kwa ustawi wa watumishi wake.