Dodoma. Mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, Jumanne Oktoba 7, 2025 ataanza kampeni zake za kusaka kura katika mikoa ya Kanda ya Ziwa huku akisisitiza kampeni za amani, umoja, upendo na mshikamano.
Akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya CCM jijini Dodoma leo Jumapili Oktoba 5,2025, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa chama hicho, Kenan Kihongosi, amesema mgombea huyo atakwenda mikoa hiyo baada ya kumaliza kampeni katika mikoa 21 ya Bara na Visiwani.
Kihongosi amesema hadi sasa Samia amefanya mikutano 77 katika majukwaa huku watu wengine wakiifuatilia mubashara kupitia vyombo mbalimbali vya habari.
Katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, Kihongosi amesema mgombea huyo atafanya kampeni zake katika mikoa ya Mwanza, Simiyu, Mara, Geita na Kagera.
Kihongosi amesema hadi sasa mgombea huyo ameendelea kunadi ilani ya chama hicho pamoja na masuala mengine, ameeleza mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wake kwa kipindi cha miaka minne aliyokuwepo madarakani ambayo ni pamoja na ukamilishaji wa miradi mikubwa ya kimkakati.
“Katika kipindi cha miaka minne, Serikali ya CCM chini ya Rais Samia imekamilisha miradi mingi na mikubwa ya kimkakati ikiwemo ujenzi mkubwa wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ambalo linazalisha megawati 2115 na limeshakamilika, ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR, daraja la Kigongo – Busisi lililopo mkoani Mwanza lililozinduliwa miezi miwili iliyopita,” amesema mwenezi huyo na kuongeza kuwa;
“Tunashukuru watanzania ambao wameendelea kujitokeza kwenye kampeni na kuonyesha imani kwa mgombea wetu, mwitikio umekuwa mkubwa inaonyesha imani ya wananchi kwake ambayo imechagizwa na uongozi unaothamini utu.”
Amesema ziara ya Kanda ya Ziwa itaanza Oktoba 7, 2025 kwa kuinadi ilani ya CCM na katika mikoa hiyo, kiongozi huyo amesema mgombea wao atakutana na makundi mbalimbali kuelezea sera na ahadi zilizopo kwenye ilani hiyo ya 2025/2030.
Kihongosi amesema katika mikoa ya Kanda ya Ziwa miradi mingi imetekelezwa ikiwemo Daraja la Kigongo- Busisi (JPM), miradi ya maji Ziwa Victoria ambayo itasambaza maji katika mikoa mingi, ununuzi wa meli, ujenzi wa vivuko na katika sekta ya uvuvi Serikali imepeleka boti ya wagonjwa kwa ajili ya kusaidia kuokoa wananchi na wavuvi.
“Mgombea amekuwa akisisitiza utu,kuthaminiana,kuheshimiana na kampeni zisizo za matusi, kejeli bali zenye kuunganisha taifa amekuwa akisisitiza amani,upendo na mshikamano. Kama watanzania tuna wajibu wa kulinda umoja tulio nao na kila mmoja wetu kuwa mlinzi wa amani,lazima tudumishe upendo,kuheshimu vyombo vya ulinzi na usalama,” amesema
Tangu kampeni zilipoanza, Samia ameifikia mikoa 21 ikiwemo mitatu ya Zanzibar akiomba ridhaa kwa Watanzania wamchague ili awatumikie kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Mikoa hiyo ni, Morogoro, Dodoma, Songwe, Njombe, Mbeya, Iringa, Singida, Tabora, Kigoma, Kusini Pemba, Kaskazini Unguja, Kusini Unguja, Ruvuma, Mtwara, Lindi, Pwani, Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara.
Kampeni za uchaguzi mkuu zilianza Agosti 28 na zitahitimishwa Oktoba 28, 2025.
Kwa mujibu wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), idadi ya Watanzania waliojiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Mpiga Kura ni milioni 37.6 ambao wataamua nani awe diwani, mbunge na Rais ifikapo Jumatano Oktoba 29, mwaka huu siku ya uchaguzi mkuu.