Miili ya waliouawa Tunduru yazikwa, polisi waendelea na msako

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma limesema miili ya watu watano waliouawa katika Kijiji cha Wenje, Kata ya Narasi Magharibi, wilayani Tunduru, imekabidhiwa kwa ndugu na tayari imeshazikwa baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Marco Chilya, akizungumza na Mwananchi leo Jumapili, Oktoba 5, 2025, amesema uchunguzi wa awali ulifanyika na kubaini chanzo cha vifo hivyo, kisha ndugu walikabidhiwa miili kwa ajili ya maziko.

“Ndugu walishachukua maiti na kuzika baada ya kufanyika uchunguzi. Hakukuwa na haja ya kuendelea kuzihifadhi hospitalini kwa kuwa dini zao hazina utaratibu wa kukaa na maiti muda mrefu,” amesema Kamanda Chilya.

Mauaji hayo yalitokea Oktoba mosi, 2025, ambapo watu watano waliuawa na wengine watatu kujeruhiwa, baada ya mvutano uliosababishwa na kupotea kwa ng’ombe wa wafugaji.

Watu hao walidaiwa kushambuliwa na kundi la wanakijiji wa Nakapunda waliokuwa wakitafuta wafugaji wanaodaiwa kumjeruhi mkulima, Hassan Moshi, aliyeshambuliwa shambani kwake na mtu ambaye hajatambulika.

Kwa mujibu wa Kamanda Chilya, majeruhi watatu bado wamelazwa katika Hospitali ya Misheni ya Mtakatifu Augustine wakipatiwa matibabu.

Amesema mpaka sasa, Jeshi la Polisi linawashikilia watuhumiwa 15 kuhusiana na tukio hilo, huku msako ukiendelea kuwabaini wengine walioshiriki.

“Uchunguzi bado unaendelea ili kuhakikisha wahusika wote wanakamatwa na kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili,” amesema.

Wakati huohuo, wakazi wa eneo hilo wameiomba Serikali kuchukua hatua za haraka kuhakikisha usalama wao, ikiwemo kuliangalia suala la kuwepo kwa wafugaji katika maeneo yao.

Wamesema ingawa kila Mtanzania ana haki ya kuishi popote ndani ya nchi, bado usalama wa wananchi na mali zao unatakiwa kupewa kipaumbele ili kuepusha matukio yanayoweza kusababisha watu kujichukulia sheria mkononi.