Sababu beki Simba kukwama Zambia

BEKI wa zamani wa Simba ya Vijana U-20, Alon Okechi Nyembe anayekipiga Zanaco FC ya Zambia amesema amechelewa kupata kibali cha kazi kilichomfanya asicheze hadi sasa.

Nyembe alicheza Simba U-20 misimu miwili kisha kupandishwa timu kubwa na alifanya mazoezi na timu hiyo pamoja na kupata nafasi ya kucheza kwenye mechi za kirafiki.

Akizungumza na Mwanaspoti, Nyembe amesema anaendelea kufanya mazoezi na timu hadi Novemba 20 mwaka huu kibali hicho kitakapotoka rasmi.

“Kulikuwa na mambo hayajakamilika ya uhamisho wangu kutoka Simba kwahiyo walipomalizana dirisha lilikuwa tayari limefungwa nimeambiwa nisubiri hadi Novemba 20 ndipo kibali changu kinatoka rasmi,” amesema Nyembe na kuongeza;

“Naendelea na mazoezi na timu ili mambo yatakapokuwa sawa niwe tayari nimefahamu timu ikoje aina yake ya uchezaji naamini mambo yatakuwa sawa na nitaanza kazi ambayo nimekuwa nikitamani kucheza nje ya Tanzania na kupata uzoefu.”

Chama la beki huyo linaongoza hadi sasa kwenye msimamo wa ligi ya Zambia inayoshirikisha timu 18, kwenye mechi saba Zanaco imeshinda nne na sare tatu ikikusanya pointi 15.