Songwe. Wananchi wa kijiji cha Nanyunyi Kata ya Ihanda, wilayani Mbozi mkoani Songwe, huenda wakapata ahueni ya muda mrefu baada Mwenge wa Uhuru kuweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha polisi kitakachohudumia zaidi ya wakazi 23,000 wa kata hiyo na vijiji vya jirani.
Jiwe hilo la msingi limewekwa leo Oktoba 5, 2025 na kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Ismail Ali Ussi ambaye amesema lengo la ujenzi wa kituo hicho ni kusaidia kupunguza matukio ya uhalifu yanayotokea mara kwa mara kwenye kata hiyo.
Amesema Serikali haitavumilia vitendo vya uhalifu na kwamba kuwepo kwa kituo hicho kutaimarisha doria na ufuatiliaji wa matukio hayo kwa haraka zaidi.
“Nimeambiwa kata hii imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya umbali kufuata kituo kikuu cha polisi Vwawa mjini, hivyo ukikamilika wananchi watapata huduma kwa haraka, na hii itasaidia pia kuongeza imani yao kwa vyombo vya dola,” amesema Ussi.
Ussi amesema kituo hicho kitakapokamilika kitumike kutoa huduma zilizohitajika za kupunguza matukio ya uhalifu na isigeuzwe kuwa mwiba kwa wananchi.
Akisoma risala ya ujenzi wa kituo hicho kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbozi, Janeth Mwambuta amesema mradi huo ulianza kutekelezwa Mei, 2025 kwa gharama za mapato ya ndani kwa kushirikiana na nguvu za wananchi.
Amesema lengo la mradi huo ni kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao, kwa kutoa huduma za kufungua majalada na kuhifadhi mahabusu kabla ya kuwapeleka mahakamani.
“Ujenzi wa kituo hicho cha polisi unatarajia kugharimu Sh140.5 milioni na nguvu za wananchi ni Sh560,000 na mpaka sasa zimetumika Sh62.7 milioni ambapo kukamilika kwake kutasaidia kusogeza huduma za kipolisi karibu na wananchi,” amesema Mwambuta.
Amesema gharama za ujenzi huo zimetokana na fedha za mapato ya ndani ya halmashauri hiyo ikiwa ni makubaliano ya baraza la madiwani kwa lengo la kuunga jitihada za Serikali ya awamu ya sita.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Hamad Mbega amesema kituo hicho cha polisi kitakapokamilika kitasaidia kupunguza matukio ya uhalifu kwenye kata hiyo ambayo imekuwa ikikumbwa na matukio ya mara kwa mara.
Aidha, baadhi ya wananchi waliohudhuria hafla hiyo walieleza kufurahishwa kwao na hatua hiyo, wakisema imekuja wakati muafaka ambapo kumekuwa na ongezeko la matukio ya wizi wa mifugo na bidhaa za wakulima.
Ester Mwazembe mkazi wa kijiji hicho ameishukuru Serikali kwa kuwakumbuka kwani wameishi muda mrefu bila kituo cha polisi karibu na sasa wanaamini hali ya usalama itakamilika.