Sura mbili ndoa za wenza kuishi mbalimbali

Mwanza. Katika zama hizi za kasi ya maendeleo ya teknolojia na uchumi, wanandoa kuishi miji tofauti kwa muda mrefu si jambo la kushangaza.

Ni kawaida kwa mfano,  kusikia mume ameajiriwa katika kampuni jijini Mwanza, huku mke akibaki Dar es Salaam kwa sababu za kazi, biashara au malezi ya watoto.

Wengine wanaishi mbali kwa sababu ya masomo, mafunzo kazini au changamoto za kifamilia. Hali hii imekuwa sehemu ya maisha ya familia nyingi mijini na vijijini.

Hata hivyo, swali kuu ni je, ndoa za aina hii zina uhai? Wataalamu wa masuala ya familia wanasema jibu ni gumu kwani maisha ya wanandoa wanaoishi mbalimbali yana faida na changamoto zake.

 Sababu za kuishi mbali                                      

Moja ya sababu kubwa ni ajira na uhamisho kazini. Wafanyakazi mara nyingi huhamishwa kutoka mji mmoja hadi mwingine.

Mara nyingi uhamisho huo haufuati mipango ya familia, na hivyo mmoja wa wanandoa hulazimika kubaki mji wa awali ili kutunza familia.

Kuna pia wale wanaotafuta elimu ya juu. Vyuo vikuu na taasisi za mafunzo ziko mijini au hata nje ya nchi, jambo linalowalazimu baadhi ya wake au waume kuondoka nyumbani kwa miaka kadhaa.

“Nililazimika kwenda Dodoma kwa miaka mitatu kusomea shahada yangu. Ilikuwa ngumu kuishi mbali na familia, lakini tuliona ni uwekezaji wa baadaye,” anasema Besta Joseph, mama wa watoto wawili.

Sababu nyingine ni biashara ambapo baadhi ya familia huchagua kuwekeza biashara katika miji tofauti ili kuongeza kipato.

Changamoto za kifamilia pia zinachangia kwakuwa wapo wanandoa wanaoishi karibu na ndugu,  ili kuwahudumia wazazi wazee, au kutokana na gharama kubwa za kuhamisha familia nzima.

Athari kwa ndoa na familia

Wataalamu wanasema, kuishi mbali kunaweza kuathiri ndoa kwa njia nyingi za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.

Wanasema kihisia, wanandoa hupoteza ukaribu wa kila siku, jambo linaloweza kuongeza upweke na msongo wa mawazo.

Kukosa kushirikiana kwenye shughuli ndogo za kila siku kula pamoja, kulea watoto, au hata mazungumzo ya kawaida, pia  kunaweza kusababisha hisia za kutengwa.

Aidha, umbali huleta hatari ya kutokuwa waaminifu. Ingawa si kila ndoa huathirika, wataalamu wanasema umbali hutoa changamoto kubwa ya majaribu, hasa pale ambapo mawasiliano hayako wazi.

“Wengi huishia kutafuta faraja kwa watu wengine wanapohisi kupuuzwa na wenza wao. Hili linaweza kusababisha kuvunjika kwa ndoa,” anasema mshauri wa mahusiano jijini Mwanza, Gifti Elias.

Anasema watoto pia huathirika kwakuwa mara nyingi mzazi mmoja hubeba mzigo mzima wa malezi, jambo linaloweza kusababisha uchovu wa kihisia na kiakili, na wakati mwingine watoto hukosa urafiki wa mzazi mmoja, hali inayoweza kuathiri maendeleo yao ya kihisia na kisaikolojia.

Kwa upande wa kiuchumi, ndoa za mbali mara nyingi ni mzigo. Safari za mara kwa mara, gharama za nyumba mbili na mawasiliano huongeza presha ya kifedha.

“Nilihamishiwa Dar es Salaam lakini familia yangu imebaki Mwanza. Kila mwezi natumia zaidi ya Sh250,000 kwa safari pekee. Ni mzigo mkubwa, lakini sina jinsi,” anasema Johakim Daniel mfanyakazi sekta binafsi.

Anasema pamoja na gharama, tangu ahame kwenye familia yake kikazi, migogoro ya ndoa imekuwa ni kitu cha kawaida kati yake na mke wake.

“Mama watoto nisiposhika simu tu ugomvi. Yaani wakati mwingine tunaweza kununiana hata wiki mbili ndiyo tunasemeshana tena. Kazi imegeuka kikwazo cha ndoa yetu. Sasa nahangaikia uhamisho kunusuru ndoa yangu,”anaongeza.

Tafiti za kimataifa zimeonesha matokeo hasi na chanya  kuhusu ndoa za mbali.

Utafiti uliofanywa Nigeria kuhusu wanandoa wanaofanya kazi ulionyesha kuwa umbali huongeza changamoto za kifamilia, ikiwemo upweke, matatizo ya kifedha na kupungua kwa ukaribu wa kimapenzi.

Utafiti wa mtaalamu wa saikolojia kutoka Idara ya Saikolojia, Chuo Kikuu cha Mercu Buana nchini Indonesia, Sonia Natasha Mirzayanti (2025) na kuchapishwa kwenye jarida la Journal of Family Sciences, ulibaini kuwa mawasiliano ya mara kwa mara kupitia WhatsApp yanachangia sana kudumisha mshikamano wa kihisia kati ya wanandoa wanaoishi mbali.

Mawasiliano hayo yakiwa na malengo, kama kushirikishana habari za familia, kupanga ratiba za likizo au kuzungumza kuhusu changamoto za kila siku, yalisaidia kupunguza upweke na kuongeza hisia za usaidizi na mshikamano.

Mirzayanti alibainisha kuwa matumizi ya teknolojia ya mawasiliano kwa umakini,  ni kiini cha kudumisha uhusiano thabiti wa kihisia.

Utafiti huo uligundua kuwa wanandoa waliokuwa na shughuli za kiroho za pamoja kama sala kwa njia ya simu au tafakari ya pamoja, walionyesha ustahimilivu mkubwa na kukabiliana na changamoto za kutokuwa pamoja, kupunguza hofu na wivu, na kujenga hisia za usaidizi wa kihisia, jambo lililoongeza uwezekano wa kudumisha ndoa zao kwa muda mrefu.

Aidha, utafiti uliochapishwa kwenye jarida la Journal of Social and Personal Relationships,  ulionyesha kuwa ndoa za mbali si lazima ziwe dhaifu zaidi ya ndoa za karibu.

Kinachobainisha ubora wa ndoa ni viwango vya uaminifu, mawasiliano na malengo ya pamoja, si umbali pekee.

Namna ya kudumisha ndoa za mbali

Mwanasaikolojia na mshauri nasihi wa uhusiano na masuala ya kijamii, Dk Michael Nyakabona anashauri wanandoa wa mbali kuweka malengo ya pamoja kuhusu mustakabali wa ndoa zao.

“Ili kudumisha uhusiano wa mbali. Cha kwanza wekeni malengo ya pamoja maana yake uhusiano wenu kesho yake ni nini? Kila mmoja ajue kesho ya uhusiano wenu yaani atambue kabisa  lengo lake ni hivi na kama kuna mipaka kwenye uhusiano wenu kila mmoja ajue mipaka yake,”anasema na kutahadharisha pia dhidi ya mawasiliano ya kupita kiasi.

“Watu wengi hudhani kwa sababu wako mbali wanapaswa kuzungumza asubuhi, mchana, jioni na siku. Hii huleta uchovu wa kihisia na huchochea wivu. Mawasiliano yawepo, lakini yawe yenye ubora na si ya uwingi,” anasema.

Anaongeza: “Kukutana faraghani mara kwa mara pia ni muhimu. Hata kama ni mara moja au mbili kwa mwaka, kunajenga ukaribu wa kihisia na kimwili. Na msisahau kufanya mambo madogo pamoja hata mkiwa mbali, kama kuangalia filamu moja kwa wakati mmoja au kushiriki ibada.’’

Anasisitiza kuepuka mazingira hatarishi hasa sehemu za burudani au sherehe zisizo na ulazima,  akieleza mara nyingi huongeza vishawishi.

Naye mshauri wa uhusiano jijini Mwanza, Gifti Elias, anaona umbali unaweza kuwa fursa ya kukua.

“Wapo wanaochukulia umbali kama adui wa ndoa, lakini wengine huutumia kujitathmini na kuboresha maisha yao. Cha msingi ni uaminifu na mipango ya baadaye.”