Pemba. Viongozi wa dini Kisiwani Pemba wamemkumbusha mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Hussein Mwinyi kutekeleza ahadi alizotoa mwaka 2020 ambazo baadhi bado hazijakamilika, huku wakimweleza kuwa yeye ndiye mwenye dhamana ya kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani bila umwagaji damu.
Akizungumza leo jumapili, Oktoba 5, 2025 katika Shule ya Utaani, Mkoa wa Kaskazini Pemba wakati wa kikao na viongozi wa dini, Dk Mwinyi amesisitiza kuwa ajenda kuu ya CCM ni kudumisha amani, mshikamano na umoja, jambo linalochangia maendeleo kuonekana kila kona ya Zanzibar.
“Pemba hii wakati wa uchaguzi uliopita hali haikuwa hivi. Hii ni neema kutoka kwa mola wetu, tuendelee kuidumisha,” amesema Dk Mwinyi.
Amesema miaka iliyopita Zanzibar ilikumbwa na ubaguzi mkubwa, lakini sasa umepungua kwa kiwango kikubwa.

“Kwa sasa watu wanachaguana kwa kuzingatia utendaji kazi na siyo asili wala dini yao,” amesema na kuongeza kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa aliyozungumza nayo mara ya kwanza marehemu Maalim Seif Shariff Hamad imechangia kudumisha mshikamano huo.
Kwa upande wao, viongozi wa dini wametoa pongezi kwa hatua zilizofikiwa lakini wakasisitiza bado kuna changamoto zinazowakabili wananchi.
Sheikh Khamis Omar wa Micheweni alisema: “Mambo mengi umeyatekeleza lakini yapo ambayo hayajafanikiwa kwa kiwango kinachotakiwa ikiwamo suala la ubaguzi kati ya Wapemba na Waunguja. Rushwa, unyang’anyi na wizi wa mazao bado vinatusumbua.”
Naye Sheikh Hafidh Saleh Hamad wa Pandani akaongeza kuwa; “Bado hali ya maisha ni ngumu. Mtu akiamka asubuhi anafikiria kula, hii ni changamoto kubwa. Simamia haki, Mungu atakulipa.”
Sheikh Abuubakar Abuubakar amesema mfumko wa bei unawaumiza wananchi na kusisitiza kuwa amani haiwezi kudumu bila haki. “Tuweke haki kwanza ndipo amani ifuate.”
Viongozi wengine walitoa maoni mbalimbali akiwamo Imamu, Omar Ali Faki kwa upande wake amesisitiza amani wakati wa uchaguzi, akisema kuna maisha baada ya uchaguzi.
Imamu Faki amesema Wazanzibari hawataki kuona watu wakipoteza maisha au kuumizwa kipindi hiki cha uchaguzi, bali watafurahi kuona amani ikitamalaki visiwani humo.
Mwenyekiti wa viongozi wa dini ya Kikristo, Nkuba Paschael amesema changamoto kubwa kwa upande wao ni ukosefu wa eneo la kuzika waumini wao wanapofariki dunia.
Naye Sheikh, Abdallah Ali Khamis ameshauri vyombo vya ulinzi na usalama kupunguza matumizi makubwa ya nguvu na badala yake, vitoe elimu kwa wananchi, huku Asia Amour Abdalarhamani wa Jumuiya ya Waislamu Pemba akilalamikia utendaji usioridhisha wa baadhi ya viongozi ngazi za Shehia.
Mohamed Abdallah Foum ameipongeza serikali kwa kuongeza mishahara na kurejesha mshikamano, lakini akaomba walimu wa madrasa na maimamu pia kupewa maslahi.
Kwa upande wake, Said Abdalla Nassor amempongeza Dk Mwinyi kwa kudumisha uzalendo na kuondoa migogoro ya kisiasa. “Tangu umeingia madarakani hakuna aliyehama nchi kutokana na migogoro. Tumepata utulivu mkubwa,” amesema.

Katibu wa Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Khalid Ali Mfaume amekumbusha kuwa amani ni jukumu la kila mmoja na si jukumu la Rais pekee.
“Viongozi wa dini tusikiingize katika siasa. Tutangulize amani na tuwe mstari wa mbele kuihifadhi,” amesema.