Wanasayansi waikubali akili unde, wakisisitiza tahadhari

Dar es Salaam. Wanasayansi wametoa tahadhari kuwa matumizi ya akili unde (AI) kama mbadala wa mtaalamu wa afya, huchelewesha wagonjwa kutibiwa na kuchangia ongezeko la usugu wa vimelea dhidi ya dawa, huku Serikali ikitoa mwongozo.

Matumizi ya akili bandia katika kujitibu, kama programu za afya ya akili au mifumo ya uchunguzi wa dalili yamekuwa yakiongezeka. Hata hivyo, wanasayansi wametaja matumizi hasi au yasiyo sahihi yanaweza kusababisha madhara kadhaa.

Wametaja utambuzi usio sahihi wa magonjwa kuwa AI inaweza kutoa majibu yasiyo sahihi au yasiyo kamili kutokana na data zisizo sahihi, ukosefu wa tathmini ya kitaalamu na kutofautisha dalili zinazofanana kama mafua na malaria.

Pia wamesema hiyo inaweza kuchelewesha huduma za kitaalamu, watu wengi huamini majibu ya AI kama tiba kamili na matokeo yake wagonjwa huacha kwenda hospitali na magonjwa yanaendelea na kuwa sugu au hatari.

Watoa huduma za afya ngazi ya jamii, watoa huduma, madaktari, viongozi, watafiti, wafamasia, wafanyabiashara na wote wanaojishughulisha na sekta ya afya 1,700 kutoka nchi 25 barani Afrika, walikubaliana matumizi ya akili unde sekta ya afya lazima yawe na usimamizi.

Akizungumza baada ya mkutano huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Tanzania Health Summit, Chakou Tindwa amesema matumizi ya teknolojia bado kuna changamoto, wanasayansi bado wana wasiwasi na matumizi ya teknolojia hiyo.

Amesema maswali ambayo wanasayansi bado wanajiuliza ni je? “Mtu anaweza kuingia katika akili unde akaweka dalili zake zikamwambia una shida hii, kapate dawa hii ni ngumu hivyo bado tunashauri eneo hili liangaliwe na kusimamiwa.

“Katika suala la utawala tutaisimamiaje ili kuhakikisha kile inachokisema basi kinakua sahihi na hatuhatarishi maisha ya watu, lakini na sisi madaktari tunapata hofu kwamba akili unde isije ikachukua kazi zetu tukawa hatuna kazi za kufanya, huu mjadala ulikuwa mkali hasa jinsi gani tunaweza kuboresha namna ya kutumia teknolojia,” amesema.

Dk Chakou ameongeza kuwa pia ni namna gani huo uboreshaji kuondoa huduma hauathiri wananchi na jinsi Serikali inaweza kuboresha na kuhakikisha ubora wa kazi zinazofanywa na akili unde, kwa kuwa kila teknolojia inavyokuja, huja na changamoto zake.

Akitoa mfano, amesema kwa sasa daktari anakwenda kwenye kliniki anakaa kuona wagonjwa, lakini kutokana na teknolojia mgonjwa anaweza kukaa nyumbani akampigia ‘video call’ akamuona akizungumza naye japo hawezi kumgusa au kumshika.

“Kwa sasa kuna mashine daktari anamwekea mgonjwa kwenye moyo, mgonjwa yuko nyumbani daktari anafuatilia. Kuna ukuaji mkubwa wa teknolojia kama telemedicine mgonjwa anaonwa kila kliniki yuko mkoani lakini daktari yuko Dar,” amesema Dk Chakou.

Akizungumza na Mwananchi, Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe amesema matumizi ya akili unde si kitu kibaya, dunia mzima inaenda huko na Tanzania haiwezi kujifungia lazima iingie huko,lakini    kwa tahadhari zote.

Amesema kuna maeneo yanatakiwa itumike na kuna maeneo haitakiwi  .

“Inaweza pia ikakupotosha usipokuwa mwangalifu, kwa mfano unapokuwa na dalili fulani unaiambia akili unde, kimsingi kwa mfano nikisema naumwa kichwa, nina homa, nakohoa…

“Kuumwa kichwa, kusikia mwili kuchoka, kuwa na homa hapo kuna magonjwa zaidi ya 100 ambayo yanaweza kusababisha maumivu ya kichwa au kupata homa, kukohoa na ndiyo maana ukiniambia hizi dalili nitakuuliza imeanza lini, unaishi wapi nataka nijue huenda changamoto hiyo inachangiwa mazingira unayoishi,” amesema.

Dk Magembe amesema kuna homa ya kifua kikuu, malaria, typhoid zinatofautiana. Hivyo mgonjwa anapokutana na daktari akamwelezea au kuzungumza naye kwenye simu ‘tele consultation’ ina maana kila mgonjwa anachojibu atamuuliza swali linalofuata na akiona majibu unayompa hayampi uhakika atakwambia tuonane.

Amesema daktari atahitaji vipimo, apime kifua au joto la mwili, “Mgonjwa huwezi kujua kwenye kifua kuna nini uiambie akili unde ili ikupe majibu sahihi. Wakati mwingine unaweza sema unasikia homa nikipima na themomita sioni, kwa sababu ili isome inatakiwa iwe imezidi joto la kawaida yaani 37.”

Hata hivyo Dk Magembe amesisitiza kuwa akili unde ina nafasi yake, lakini haiwezi kuondoa umuhimu wa kusikilizwa na daktari au mtaalamu wa afya.

“Na akili unde inaweza pia ikakupotosha kwa sababu mpaka ikwambie una tatizo fulani inabidi iunganishe matukio mbalimbali.”

Kuhusu akili unde kufanya vizuri katika kuangalia majibu ya vipimo mbalimbali kama XRay na CT Scan kwa sababu tayari daktari wa kubaini alitangulia awali.

“Matumizi ya akili unde kwenye sekta ya afya tunayakaribisha, tumeshayaanza lakini lazima tuchukue tahadhari zote usije ukaenda kutibu kitu sicho na kinachotugharimu kwa sasa ni usugu wa dawa na sababu mojawapo ni kujitibu,” amesema.

Amesema wagonjwa wengi hutumia akili unde, wanaenda kununua dawa sizo matokeo yake wanachelewa kubaini ugonjwa.

unakwenda mwenyewe huna uhakika unanunua dawa lakini kumbe kinachokusumbua siyo hicho, maendeleo ya teknolojia tunayataka lakini lazima twende na tahadhari

Pamoja na hayo, wanasayansi hao walijadili mambo matatu makubwa ikiwemo matumizi ya takwimu, teknolojia na huduma ya afya kwa wote.

Upande wa takwimu walisema kumekuwa na mafanikio makubwa na uwepo wa mifumo mingi ya kukusanya data lakini katika mjadala imeonekana kuna mifumo michache sana inayohusika katika kukusanya data za afya.

“Imeonekana itakuwa jambo jema kama sekta binafsi na Serikali watatumia mfumo mmoja kukusanya data, kupitia mfumo huu kama mtu atakaa pale Wizara ya Afya akitaka kupata data ya hospitali binafsi iliyopo Tandahimba, akiingia kwenye mfumo aone leo wameenda wagonjwa wangapi, wamebainika kuumwa nini na wamepata huduma gani,” amesema Dk Chakou.

Katika upande wa afya kwa wote, wanasayansi hao wamesisitiza lazima mfumo uwe wazi namna gani wananchi watapata huduma kwa urahisi, waweze kumudu gharama na ubora stahiki.