Zijue aina za uongo kwenye mapenzi

Dar es Salaam. Wapo watu wanaoamini kwamba, endapo kusema ukweli kunaweza kuumiza, basi kusema uongo huwa ni njia mbadala inayokubalika katika mazingira fulani.

Katika utafiti mbalimbali wa kihisia na kisaikolojia, watafiti wameendelea kujiuliza: kwa nini watu husema uongo? Imebainika kuwa uongo husemwa katika mazingira tofauti kwa sababu mbalimbali.

Wengine hudanganya ili kuficha makosa waliyojua kwamba hayakubaliki kijamii au kimaadili; wengine hudanganya ili kumlinda mtu mwingine asijeruhiwe kihisia; na wapo wanaosema uongo ili tu kuficha hisia au tamaa zao binafsi wasije wakahukumiwa.

Japo uongo unaweza kuwasilishwa kwa njia ya ‘nia njema’, bado haupotezi asili yake ya kuwa si kweli. Wapo wanaojitetea kwamba uongo uliolenga kumkinga mtu dhidi ya maumivu si uongo mbaya bali ni njia ya kuchelewesha ukweli, yaani ukweli ambao utasemwa siku moja. Lakini ukweli unabaki kuwa uongo hauna rangi nzuri,  bado ni kuvuruga uhalisia.

Mfano wa wazi ni siasa. Wanasiasa mara nyingi wamekuwa wakihusishwa na uongo kupitia ahadi zisizotekelezeka.

Katika vipindi vya kampeni, baadhi yao hutoa ahadi zinazopendeza na kutia matumaini, lakini muda mfupi baadaye wananchi hugundua kwamba hawakuwa wakielezwa ukweli.

Lakini, je, waongo ni wanasiasa pekee? Ukweli ni kwamba uongo umeota mizizi katika maeneo mengi ya maisha ya kila siku, na moja kati ya maeneo yanayokithiri ni katika mapenzi.

Katika uhusiano wa kimapenzi, uongo umetumika sana  si mara moja au mbili bali ni jambo linalojirudia na kwa sura tofauti. Baadhi ya uongo huonekana dhahiri tangu mwanzo, lakini aina nyingine za uongo huja kwa sura ya ukweli na hudumu kwa muda mrefu kabla ya kugundulika.

Kuna uongo ambao hadi leo bado haujafichuka kwa yule aliyedanganywa, japokuwa aliyesema anajua ukweli mzima. Mara nyingine watu wawili hukaa pamoja, kucheka na kushirikiana maisha, huku mmoja wao akiwa na siri nzito moyoni na mwingine akiamini kila kitu kinachoendelea ni cha kweli.

Swali linalobaki ni: umedanganywa mara ngapi bila kujua? Na utaendelea kudanganywa hadi lini?

Kutoka katika muktadha wa saikolojia, kuna maeneo kadhaa yanayotajwa kuwa chanzo kikuu cha uongo miongoni mwa wapenzi.

Moja ya maeneo hayo ni pale inapokuja suala la muda wa kuwa pamoja. Wakati mapenzi yanaanza, wapenzi wengi hupenda kutumia muda mwingi pamoja, wakitoka, wakizungumza, na hata kushiriki tendo la ndoa mara kwa mara.

Hali hii hubadilika baadaye, hasa pale mmoja (hasa mwanaume) anapopunguza muda wa uwepo wake. Hapo ndipo visingizio huanza,  kazi zimeongezeka, vikao havikomi, safari zimekuwa nyingi.

Lakini kiuhalisia, sababu hizi huwa si za kweli, bali ni pazia linalofunika ukweli wa kupungua kwa motisha au hata uwepo wa mtu wa tatu.

Zaidi ya hapo, kuna uongo unaojitokeza wakati mmoja wa wapenzi anapojaribu kuficha hisia zake halisi. Wapo wanaofikiria wapenzi wao wa zamani hata wakati wakiwa katika tendo la ndoa na mpenzi wa sasa.

Wengine huvutiwa na watu wengine mitaani lakini hukataa kata kata walipoulizwa, wakihofia kuumiza hisia za wenzao.

Kwa hofu ya madhara ya kihisia, huchagua kusema uongo  si kwa sababu hawajui ukweli, bali kwa sababu hawataki ukubalike.

Katika nyanja nyingine nyeti, wanaume wengi husema uongo kuhusu tabia ya kujichua.

Wapo wanaofanya hivyo hata wakiwa kwenye uhusiano, lakini hawawezi kukiri wanapoulizwa. Wengine huenda mbali zaidi na kudanganya kuhusu hisia zao za kutamani kufanya ngono kinyume na maumbile, wakihofia kuonekana wa ajabu au wasio na maadili.

Hata wakikiri wamewahi kuhusika na aina hiyo ya ngono, mara nyingi ni baada ya kugundulika au kushinikizwa, na si kwa hiari yao.

Eneo lingine linaloongopewa kwa kiwango kikubwa ni kuhusu idadi ya wapenzi wa zamani. Wengi huona aibu au kuogopa kupoteza nafasi mbele ya mpenzi mpya, hivyo huchagua kuficha au kupunguza idadi.

Utasikia mtu akisema amewahi kuwa na mpenzi mmoja tu, wakati ukweli ni kuwa idadi ni kubwa zaidi. Siku zinavyoenda, mtu huanza kugundua jina baada ya jina, kumbukumbu baada ya kumbukumbu, hadi ukweli unaanza kujionyesha kwa vipande.

Ni kweli kuwa si kila uongo huja kwa nia mbaya. Wengine hudanganya wakiamini wanawalinda wapendwa wao. Lakini ni vyema kukumbuka kuwa uongo, hata ule wa nia nzuri, una gharama. Wapo walioteseka, walioumizwa, na waliopoteza imani kwa sababu ya uongo wa mapenzi.

Kwa hivyo, ni wakati wa kujitafakari. Umeficha nini? Umewahi kudanganywa kwa kiasi gani? Na je, umejiandaa vipi kupambana na ukweli siku utakapowadia? Kwani hata ukweli ukichelewa, siku moja hufika.