Baada ya kurejea mzigoni Yanga, Folz atoa tamko

KOCHA Mkuu wa Yanga, Romain Folz amerejea nchini kuendelea na majukumu licha ya kuwepo kwa presha kubwa kwa mashabiki na hata mabosi kutaka apigwe chini, lakini ratiba ambayo anataka kuanza nayo itawatoa jasho mastaa wa timu hiyo.

Folz alitimkia Afrika Kusini alikoenda kwa safari binafsi baada ya kutoa mapumziko ya siku tatu kwa wachezaji na viongozi wa benchi la ufundi iliyoisha wikiendi iliyopita.

Folz amerejea Oktoba 4, 2025, kisha Oktoba 6,2025 ameliamsha kwa kuendelea na mazoezi akigawa dozi za maana kwa kikosi hicho ambayo yalikuwa na vipindi viwili tofauti huku akisema kilichotokea mechi iliyopita dhidi ya Mbeya City wamesahau na kusonga mbele.

Kocha huyo ameanza na ratiba ya uwanjani asubuhi ikifanyika pale kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge jijini Dar, akitumia saa mbili na robo kuwaandaa wachezaji wa kikosi hicho kinachojiandaa na mechi za raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Silver Strikers ya Malawi.

YANG 01


Katika mazoezi hayo, Folz licha ya presha ya nje ya uwanja, lakini hakuonyesha kinachopungua akiendelea na majukumu kama kawaida, huku akionyesha kusisitiza juu ya umakini.

Kocha huyo alikuwa na awamu ya pili ya mazoezi jioni yakifanyika hapo hapo akisema ratiba hiyo itakwenda kwa siku tatu hadi nne akitaka kuwaongezea ubora wachezaji wa kikosi hicho kinachoshika nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu Bara inayoongozwa na Simba yenye pointi sita sawa na Singida Black Stars, ila ikibebwa na mabao ya kufunga na kufungwa zikifuatiwa na JKT Tanzania yenye tano.

Mastaa wote wa timu hiyo kasoro wale waliokwenda kujiunga na timu za taifa walishiriki ratiba hiyo huku kocha huyo akichukua wachezaji wachache kutoka timu ya vijana.

YANG 02


Hata hivyo, kocha msaidizi wa timu hiyo, Manu Rodriguez hakuwa sehemu ya mazoezi ya asubuhi, ambapo Mwanaspoti linafahamu kwamba raia huyo wa Hispania aliomba ruhusa maalumu kurudi kwao kwa mambo binafsi kisha atarejea.

Akizungumzia kurejea kwake, Folz mwenye uraia wa Ufaransa alisema licha ya kupata sare isiyo ya mabao katika mechi ya mwisho wa Ligi dhidi ya Mbeya City, matokeo hayo hayawaondoi kwenye malengo yao ambapo yatakwenda kuwaimarisha.

YANG 04


Folz amesema ligi bado mbichi na kwamba anaamini kikosi chake kitarudi katika njia ya ushindi kwenye mechi zijazo za Ligi, huku akiwasubiri wachezaji waliokwenda kujiunga na timu za taifa.

“Kupata sare ni matokeo ya soka, kuna wakati unashinda na kuna wakati unaweza kupoteza, ingawa sio aina ya matokeo ambayo mashabiki wetu wanapenda kuyaona, tumerudi kazini tunaendelea kujipanga, hatuwezi kuendelea kulalamika,” amesema Folz na kuongeza:

YANG 03


“Tutabadilisha hili tunajua tulianguka kwa kwasababu gani na tufanye nini kurekebisha, ligi bado mbichi tuna safari ndefu kitu cha muhimu ni kuendelea kuimarika kwa wachezaji wangu kadiri ya muda unavyosogea.” 

Wakati kocha akisema hayo, Oktoba 7, 2025 ndio iliyoelezwa ingekuwa siku ya vigogo wa Yanga kukutana ili kujadili hatma ya kocha huyo, ikielezwa mtu pekee anayeweza kumbakisha au kuridhia msimamo wa baadhi ya viongozi kumuondoa klabu ni Rais Injinia Hersi Said aliyekuwa nje ya nchi.

YANG 05


Mashabiki na baadhi ya viongozi wanamlalamikia Folz kwa kuifanya timu hiyo kucheza bila kuvutia tofauti na ilivyozoeleka licha ya kwamba katika mechi 10 alizoiongoza zikiwamo tano za mashindano na za kirafiki haijapoteza, huku ikishinda tisa na kutoka sare nane ikifunga mabao 21 na kufungwa mawili.