Bweni lingine lateketea kwa moto Kilimanjaro, wanafunzi zaidi ya 90 wanusurika

Rombo. Zaidi ya wanafunzi 90 wa Shule ya Sekondari Mkuu iliyopo Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro wamenusurika kuungua baada ya bweni walilokuwa wakilala kuteketea kwa moto leo Oktoba 6, 2025 wakati wakiwa ibadani.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Kilimanjaro, Jeremiah Mkomagi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo leo wakati wanafunzi hao wakiwa kwenye ibada ya asubuhi.

Aidha, Kamanda Mkomagi amesema wanaendelea kuchunguza chanzo cha moto huo. “Hakuna madhara ya kibinadamu zaidi ya uharibifu wa mali uliojitokeza. “Taarifa za awali zinaonesha moto ulianza saa 11:30 alfajiri wakati wanafunzi wakiwa katika sala ya asubuhi, ilipofika saa 1:29 asubuhi ndipo tulipokea taarifa ya tukio hilo la moto na tulifika eneo la tukio,” amesema Kamanda Mkomagi.

Aidha, amesema mali zilizoteketea katika jengo hilo lenye vyumba viwili ni magodoro 91, vitanda 46, nguo za wanafunzi, madaftari. “Kwa ujumla vitu vyote vinavyotumiwa na wanafunzi hao hakuna kilichookolewa.

Amesema katika ajali hiyo ya moto hakuna majeruhi wala vifo, huku akiwasisitiza wananchi kuchukua tahadhari na kuripoti matukio ya moto mapema ili kupunguza madhara.