CRDB yatoa Sh5 bilioni kuwakwamua wajasiriamali kiuchumi

Mbeya. Jumla ya Sh5 bilioni zimetumika kuwakwamua kiuchumi wajasiriamali wadogo 2,000 kupitia kampuni tanzu ya CRDB Foundation kwa kipindi cha miezi sita.

Mbali na wajasiriamali hao, makundi mengine yaliyofikiwa na huduma ya benki hiyo ni wanafunzi kuanzia elimu ya msingi hadi chuo kikuu, walimu, watumishi wa umma na sekta binafsi ikiwa ni sehemu ya mafanikio kwa taasisi hiyo ya kifedha.

Akizungumza leo Oktoba 6, 2026 wakati wa hafla ya kuadhimisha wiki ya huduma kwa mteja, Meneja Biashara wa Benki ya CRDB Nyanda za Juu Kusini, Domina Mwita amesema hadi sasa wanajivunia kuwafikia wananchi wengi kwa huduma bora na za haraka.

Amesema kupitia kampuni tanzu ya CRDB Foundation, zaidi ya wajasiriamali 2,000 wamenufaika na mikopo ya Sh5 bilioni isiyo na dhamana ambazo zimewainua kiuchumi kwa mtu mmojammoja.

Amesema katika kuhakikisha benki hiyo inawafikia wananchi wengi zaidi, imejipanga vyema kutokana na maboresho ya mifumo kidijitali akieleza kuwa walimu, wanafunzi, watumishi wa umma na sekta binafsi wamefikiwa.

“Hii ni kutokana na kuaminiwa na wateja wetu, kufuatia huduma zetu kukubalika, tumeboresha mifumo ambapo mwanafunzi, mwalimu na mtu yeyote anaweza kupata huduma popote kupitia simu yake,” amesema Domina.

Kwa upande wake, meneja wa benki hiyo tawi la Mwanjelwa, Singwa Mwenemilao amesema wiki ya huduma kwa mteja inaenda sambamba na miaka 30 ya kuwapo kwa benki hiyo.

Amesema kwa kipindi hicho wanaendelea kutoa huduma bora na kuunganisha mifumo kwa ubunifu ili kumhakikishia mteja kupata huduma kwa ubora na haraka popote alipo.

“Ili kuhakikisha tunaendelea kutoa huduma bora, tumeboresha na kuunganisha mifumo yote kidijitali kwa ubunifu, wiki hii inaenda sambamba na miaka 30 tangu kuanzishwa Taasisi hii,” amesema Singwa.

Akitoa salamu za Serikali, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Justice Kijaji amesema benki hiyo imekuwa sehemu ya maendeleo kwa jamii kwa kugusa makundi yote na huduma zake zimekuwa chachu kiuchumi.

“Serikali imeendelea kuiamini benki hii na kwa kuanzia, tayari tumenunua posi 100 za kukusanyia ushuru zitakazounganishwa na CRDB ili kuongeza makusanyo, kwa ujumla tunatambua na kuthamini mchango wenu kwa kuwa tumeona huduma inapatikana kila kona hadi kufika nje ya nchi,” amesema Kijaji.

Mmoja wa wajasiriamali, Debora Kalomo amesema mafanikio yake yamechagizwa zaidi na benki hiyo licha ya woga aliokuwa nao katika mikopo, lakini alipewa elimu na watoa huduma na sasa amekuwa sehemu ya wanufaika.

“Nilianza kwa kuchechemea sana biashara zangu lakini nilishawishiwa kuchukua mkopo ambao awali niliogopa lakini nilipewa elimu na sasa naweza kuendesha shughuli zangu kupitia kampuni ya D Events,” amesema Deborah.

Naye Obedi Mtweve amesema benki hiyo imekuwa sehemu ya dira ya maendeleo kwa wananchi kwa kugusa makundi mbalimbali kwa huduma zinazokubalika kiushindani ndani na nje.

“Sisi wafanyabiashara tumekuwa sehemu ya mafanikio ya miaka 30 ya benki hii, mikopo tunayochukua imekuza uchumi, tunaomba mfike hadi China ambapo ndio wengi tunachukua bidhaa,” amesema Mtweve.