Moshi. Mkuu wa Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, Raymond Mwangwala ametoa wito kwa watafiti nchini kufanya utafiti wa kisayansi kuhusu uhusiano uliopo kati ya matumizi ya kahawa na umri wa kuishi kwa binadamu (life span), akisema huenda wazee wengi wa vijijini wameishi umri mrefu kutokana na unywaji wa kahawa.
Kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2022, Mkoa wa Kilimanjaro ni miongoni mwa mikoa yenye idadi kubwa ya wazee, huku Wilaya ya Rombo ikitajwa kuongoza.
Akizungumza leo Oktoba 6, 2025 wakati wa kufunga Tamasha la Kahawa (Kahawa Festival 2025) msimu wa sita, lililofanyika kwa siku tatu mjini Moshi, Mwangwala amesema uzoefu alioupata katika wilaya hiyo umeonyesha kuwa matumizi ya kahawa huenda yana mchango katika kuongeza umri wa maisha ya binadamu.
“Wiki tatu zilizopita nilihudhuria mazishi ya wazee watatu wenye umri wa zaidi ya miaka 100, mmoja 115, mwingine 105 na mwingine 102. Hili limenifanya nijiulize je, matumizi ya kahawa yanaweza kuongeza muda wa kuishi? Nawaachia watafiti watupatie majibu,” amesema.
Amebainisha kuwa inawezekana wazee katika wilaya hiyo wanaishi umri mrefu kutokana na utamaduni wao wa kunywa kahawa mara kwa mara, hivyo akashauri jamii iache dhana potofu kuhusu kinywaji hicho maarufu duniani.

Mkuu wa Wilaya ya Rombo Raymond Mwangwala (Kulia) akicheza Draft na Mkurugenzi mkuu wa Bodi ya kahawa Tanzania (TCB) Primus Kimaryo katika moja ya vijiwe vya kahawa vilivyokuwepo katika Tamasha la kahawa 2025 lililofanyika kiwanda cha kukoboa Kahawa (TCCCO) mjini Moshi.
Ameeleza kuwa kahawa ni kinywaji cha pili kwa matumizi duniani baada ya maji ambapo kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Kahawa (ICO), vikombe bilioni tatu hunywewa kila siku na kwamba kwa takwimu hizo, Tanzania inajivunia kuwa sehemu ya uchumi mkubwa wa dunia kupitia zao hilo la kimkakati.
Hata hivyo, amebainisha kuwa licha ya umaarufu huo, soko la ndani la kahawa bado ni dogo kutokana na dhana potofu kuwa kinywaji hicho ni hatari kiafya.
“Ukweli ni kwamba kahawa ina faida nyingi kiafya, ikiwemo kuchangamsha mwili,” amesema.
Amefafanua kuwa kahawa, pia, ni kivutio cha kijamii nchini hasa katika maeneo ya pwani ambako vijiwe vya kahawa huleta watu pamoja kwa mijadala na kubadilishana mawazo, hivyo kuwa sehemu ya tiba ya msongo wa mawazo.
Pia, amewahamasisha vijana kuchangamkia fursa za ajira katika mnyororo wa thamani wa kahawa, ikiwemo uandaaji, uonjaji na usindikaji, akisema kahawa ni “dili kubwa” la kiuchumi.
Mwenyekiti wa Bodi ya Kahawa nchini, Profesa Aurelia Kamuzora amevitaka vyama vya ushirika kote nchini kuhamasisha wakulima wa kahawa kupanda miti kati ya mashamba yao kama njia mojawapo ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Amesema hatua hiyo ni muhimu ili kuhakikisha kuwa katika miaka ijayo, kahawa ya Tanzania inaendelea kushindana vyema katika soko la dunia, hasa ikizingatiwa kuwa masoko mengi sasa yanatoa kipaumbele kwa bidhaa zinazozalishwa kwa kuzingatia mazingira.
“Vyama vya ushirika vihimize wakulima kupanda miti kwenye mashamba ya kahawa ili tupambane na mabadiliko ya tabianchi, lengo ni kuhakikisha kwamba miaka ijayo tunakuwa na nafasi nzuri katika masoko yanayothamini jitihada za kupambana na mabadiliko ya tabianchi, kwa hiyo, hakuna kulala,” amesema Profesa Kamuzora.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), Primus Kimaryo amesema wananchi wameonyesha mwitikio mkubwa katika kuendeleza zao hilo, jambo ambalo limewasaidia sio tu kujiongezea kipato, bali pia kubuni njia mpya za matumizi ya kahawa katika maisha ya kila siku.
“Kwa sasa, tunashuhudia mabadiliko makubwa kwenye tasnia ya kahawa, hatuzungumzii tu kuongeza thamani kama kinywaji, bali pia matumizi mengine kama vile kutengeneza mafuta ya kujipaka, ‘coffee scrubs’, na bidhaa nyingine nyingi zitokanazo na zao hilo,” amesema Kimaryo.
Meneja masoko wa chama kikuu cha ushirika mkoani Kagera (KDCU), Abertus Paschal amesema wamejipanga kuhakikisha wakulima wanapata masoko yenye ushindani wa kimataifa ili wazalishe kwa tija.
“Maonyesho haya yanatusaidia kutuunganisha kama daraja kati ya wakulima wa wilaya zetu na kufikia wanunuzi, Tanzania tunauza kahawa Japan, Indonesia sasa hivi tunachangamkia soko jipya la China ambalo walikuwa hawajui kahawa kwa undani, lakini sasa hivi tunaona wamekuwepo baadhi ya raia wa hizo nchi,” amesema Paschal.
Amesema: “Mpaka sasa chama chetu kina wakulima 64,000 na ili waone kahawa yao ina thamani, tunatafuta masoko yenye ushindani.”
Naye mwenyekiti wa tamasha hilo, Dennis Mahulu amesema zaidi ya watu 2,000 wameshiriki, ambapo wamepata fursa ya kufundishwa namna ya kuhudumia zao hilo kutokana na sheria mpya ya Umoja wa Ulaya (EU) kwamba kahawa inayozalishwa kutokana na ukataji wa miti haitaingia Ulaya.