Leo tunapoanza Wiki ya Huduma kwa Wateja ya mwaka 2025 chini ya kauli mbiu “Dhamira: Inawezekana,” najikuta nikitafakari kwa kina maana ya wakati huu kwa Mwananchi Communications Limited (MCL), na kwangu binafsi kama mtu niliyekabidhiwa kuongoza jahazi hili.
Hii si Jumatatu ya kawaida. Ni mwanzo wa maadhimisho ya kimataifa ya ubora wa huduma, na pia ni hatua muhimu katika safari yetu, kwa kuwa MCL inatimiza miaka 25 tangu kuanzishwa kwake.
Haya yote kwa pamoja yanatukumbusha ukweli huu: wateja si sehemu tu ya simulizi yetu, bali wao ndio sababu kuu ya sisi kuwapo.
Aprili 29, 2025 ilipotangazwa rasmi uteuzi wangu kuwa Mkurugenzi Mtendaji, niliguswa na mwitikio mkubwa kutoka kwa familia ya MCL, Bodi, wafanyakazi wenzangu na umma kwa ujumla.
Kilichonishangaza zaidi ni upeo wa matokeo ya tangazo hilo: viongozi wa Serikali na wabunge walituma pongezi za dhati, viongozi wa biashara walionyesha ukarimu wao, na Watanzania wa kawaida kama wasomaji na wafuasi wetu, walituma ujumbe wa aina mbalimbali wa kutia moyo na matarajio.
Joto la sauti hizo lilinikumbusha kwamba nafasi hii si ya mtu mmoja; ni safari ya pamoja ya kuaminiana, kuhudumiana na kubadilika. Wakati huo haukuwa salamu ya kukaribishwa pekee, ulikuwa pia ni agizo la kuongoza kwa uhalisia na kuweka wateja wetu katikati ya kila kitu tunachofanya.
Nilipokubali jukumu la kuongoza MCL, ukweli mmoja ulidhihirika mara moja: nafasi hii si ya kusimamia shughuli, takwimu au mikakati pekee. Ni jukumu la kulinda na kuimarisha urithi wa miaka 25 wa kuaminiana kati ya MCL na watu wa Tanzania, na hata nje ya mipaka, wanaotutegemea kila siku kupata habari, msukumo na mawasiliano.
MCL ilipoanzishwa robo karne iliyopita, mazingira ya habari yalikuwa tofauti sana na jinsi yalivyo leo. Magazeti ya kuchapishwa yalitawala, yale ya kidijitali yalikuwa yanapenyeza taratibu, na hadhira ilikuwa ikishiriki kwa namna rahisi na inayotabirika.
Miaka ikapita, teknolojia, majukwaa na mienendo ya wateja vikabadilika, lakini jambo moja limebaki thabiti nalo ni imani ya wateja wetu.
Bilionea Warren Buffett aliwahi kusema: “Inachukua miaka 20 kujenga sifa na dakika tano tu kuibomoa. Ukifikiria hilo, utafanya mambo kwa namna tofauti.” Kwa miaka 25, MCL imejenga sifa yenye misingi ya uadilifu, ukweli na huduma kwa jamii.
Kila msomaji mwaminifu anayenunua Mwananchi asubuhi na mapema, kila mtaalamu anayesoma The Citizen mtandaoni, kila mtunga sera anayerejea habari zetu za Bunge, na kila mtangazaji aliyetuamini kwa chapa yake; kila mmoja amejenga taswira tuliyo nayo leo.
Simon Sinek anakumbusha katika msemo wa Anza na Kwanini: “Watu hawanunui kile unachofanya; wananunua kwa nini unakifanya.” Kwa miaka 25, “kwanini” ya MCL imekuwa rahisi: kuelimisha, kufundisha na kuwawezesha watu, huku tukitanguliza mbele mahitaji yao. Mikutano hii, iwe ni kupitia gazeti la kuchapishwa, majukwaa ya kidijitali au ana kwa ana, ndiyo mapigo ya moyo ya taasisi yetu.
Nakumbuka vizuri tukio moja mwezi Mei, wiki chache tu baada ya kuingia ofisini. Nilimtembelea muuzaji wetu wa muda mrefu jijini Dodoma, mtu ambaye ameuza magazeti kwa zaidi ya miaka 10.
Tulipokuwa tumesimama kwenye kibanda chake kidogo, alisimulia hadithi za wateja waliokuwa wakifika kila siku, wengine kwa zaidi ya miaka 10, wakitegemea magazeti yetu kama sehemu ya ratiba ya kila asubuhi. Alitabasamu na kusema: “Magazeti yenu si bidhaa tu; ni sehemu ya maisha ya kila siku ya watu.” Kauli hiyo rahisi ilinipenya moyoni. Ilinikumbusha kwamba ukweli na uthabiti ndiyo msingi wa uhusiano wa kudumu.
Wiki hiyo hiyo nilizungumza na kijana mjasiriamali aliyekuwa ametangaza biashara yake ndogo kupitia majukwaa yetu ya kidijitali. Aliniambia jinsi tulivyomsaidia kufikia wateja ambao hangeweza kuwafikiria kabisa.
Wakati huohuo, nilihudhuria moja ya matukio makuu ya MCL—Mwananchi Thought Leadership Forum, ambapo nilikutana na mamia ya washiriki na wadau waliokuwa wamenufaika na programu zetu.
Mazungumzo haya na wauzaji, watangazaji, wasomaji, washirika, watunga sera na wanajamii yalinikumbusha jambo la msingi: huduma si ununuzi tu, bali ni athari za kibinadamu.
Kauli mbiu “Dhamira: Inawezekana” haingekuwa na maana zaidi kuliko ilivyo sasa kwa MCL. Kukibadilisha chumba cha habari cha magazeti ya jadi kuwa taasisi ya vyombo vya habari yenye kipaumbele cha kidijitali, kulionekana ni ndoto kubwa.
Lakini leo hii tupo hapa, tukiwa na majukwaa ya kidijitali yenye mafanikio, jamii shirikishi na uhusiano thabiti zaidi na hadhira yetu.
Mabadiliko haya hayakutokea kwa bahati. Yamewezekana kwa sababu ya wateja waaminifu waliotuwezesha kubadilika pamoja nao, na kwa sababu ya timu yetu iliyojitolea na kuamini katika dhamira hii. Kauli ya Sinek inatukumbusha kwamba lengo ndilo husukuma vitendo.
“Kwanini” yetu hutusukuma kutoa huduma bora kila mara, kuendelea kubuni, na kuweka mteja katikati ya kila uamuzi tunaofanya.
Kwa MCL, huduma kwa wateja si idara, ni utamaduni. Ipo kwa wahudumu wa usambazaji wanaoamka kabla hakujapambazuka ili kusambaza magazeti Tanzania nzima.
Ipo kwa wasimamizi wa kidijitali wanaojibu maelfu ya maswali mtandaoni kwa uvumilivu. Ipo kwa wahudumu wa kituo cha mawasiliano wanaoshughulikia maswali kwa huruma.
Ipo pia kwa waandishi wetu, wahariri na timu za matukio wanaounda maudhui na matukio yenye maana. Hawa wote ndio mashujaa wasiotangazwa tunaowasherehekea leo.
Kama miaka 25 ya mwanzo ya MCL ilikuwa ya kujenga imani, basi miaka 25 ijayo itakuwa ya kuizidisha. Tunajiuliza maswali makubwa: Tunawezaje kusimulia habari ambazo si za kuarifu tu bali pia za kuwawezesha?
Tunawezaje kutumia teknolojia kuhudumia badala ya kukwamisha? Tunawezaje kuhakikisha ushirikishwaji, ili kwamba popote ulipo, Dar es Salaam, Arusha, Dodoma au nje ya Tanzania, maudhui ya MCL yakuzungumzie?
Majibu yako katika ubunifu, huruma na usikivu. Kama nahodha wa jahazi hili, jukumu langu ni kuhakikisha kwamba kila jukwaa jipya, kila simulizi na kila huduma mpya inaimarisha imani iliyotutambulisha kwa miaka 25. Kila uamuzi huanza na wateja wetu, na kila hatua mbele huelekezwa na “kwanini” ya kila tunachofanya.
Katika siku hii ya kwanza ya Wiki ya Huduma kwa Wateja ya 2025, nataka kusimama na kusema asante. Kwa wateja wetu: ninyi ndio dira yetu, wakosoaji wetu, wapiga debe wetu na washirika wetu. Ninyi ndio mliofanya miaka 25 iliyopita iwezekane, na ninyi ndio mtafanya miaka 25 ijayo kuwa na maana zaidi.
Kwa wafanyakazi, ninyi ni watu wa thamani kubwa: kujitolea kwenu, ubunifu wenu na uvumilivu wenu kumefanikisha dhamira yetu kila siku. Ninyi ndio mapigo ya moyo wa MCL, na ni kwa sababu yenu wateja wetu wanahisi kuonekana, kusikilizwa na kuthaminiwa.
Leo tunasherehekea si kwa maneno pekee, bali kwa vitendo. Kwa sababu kwa MCL, dhamira yetu daima imekuwa, na itaendelea kuwa, inawezekana kwa sababu ya ninyi.
Kama nahodha, najua kipimo cha kweli cha uongozi wangu kitakuwa ni jinsi tunavyowahudumia ipasavyo wale wanaotuamini zaidi yaani wateja wetu.
Wiki njema ya Huduma kwa Wateja.