Dk Nchimbi ahitimisha kampeni Tabora akiahidi viwanda

Tabora. Mgombea mwenza wa urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amehitimisha siku tatu za kampeni mkoani Tabora huku akiahidi ujenzi wa viwanda vya utafiti wa mbegu za kilimo, tumbaku na cha mbolea.

Katika mikutano hiyo iliyofanyika majimbo sita ya mkoa wa Tabora kuanzia Oktoba 4 hadi leo Jumatatu, Oktoba 6, 2025, Dk Nchimbi amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, kumchagua Samia Suluhu Hassan awe Rais, wabunge na madiwani.

Mikutano hiyo katika majimbo hayo ambayo Samia hakuyafikia, Dk Nchimbi alieleza yatakayofanyika miaka mitano ijayo iwapo watachaguliwa huku wagombea ubunge wao wakibainisha mafanikio ya miaka mitano iliyopita.

Sekta za afya, elimu, miundombinu ya barabara na madaraja, kilimo, ufugaji na maji ni maeneo ambayo yameelezwa yalivyofanyika na yatakayofanyika chini ya Serikali ya CCM.

Dk Nchimbi amehitimisha ziara hiyo kwa kumwaga ahadi kadhaa na kueleza kwa nini CCM inafaa kuendelea kushika dola. Baada ya Tabora sasa atasafiri hadi mkoani Pwani kuendelea kutafuta ushindi wa chama hicho.


Aidha, Dk Nchimbi amesimikwa kuwa msaidizi wa Mtemi, kimila akiitwa ‘Mtongi’ baada ya mkubwa wake mtemi Hangaya ambaye ni Raisi Samia Suluhu Hassan.

Tukio hilo limefanyika katika Uwanja wa mpira Kigwa, Jimbo la Igalula, Mkoa wa Tabora na kupewa jina la Nyungu ya Mawe.

Aliyeongoza tukio la kumsimika ni Mwenyekiti wa Machifu Mkoa wa Tabora na Makamu Mwenyekiti wa Machifu Tanzania, Msagata Fundikila.

Dk Nchimbi ameahidi ujenzi wa kiwanda cha tumbaku  ili kupunguza gharama za usafirishaji lakini kuchagiza ajira kwa vijana.

Amesema Mkoa wa Tabora unazalisha tumbaku kwa asilimia 60 ya Tumbaku yote inayozalishwa nchini ambapo Sikonge ni miongoni mwa maeneo yanayolima Tumbaku kwa wingi.

“Katika ilani ya CCM, tumeahidi kuendeleza ushirikiano na taasisi mbalimbali kuhakikisha wakulima wa tumbaku wanapata haki yao. Tunataka tumbaku ya Sikonge iwe kichocheo kikuu cha maendeleo kwa watu wake,” amesema Dk Nchimbi.

Viwanda vingine ambavyo Dk Nchimbi ameahidi kutekelezwa iwapo CCM itashinda ni kiwanda cha utafiti wa mbegu za kilimo pamoja na cha mbolea ili kuwafanya wakulima kulima kwa tija.

Katika mkutano wa leo, Dk Nchimbi amewaeleza wananchi wa Tabora hususan wa jimbo la Ugalula kwamba ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) unakwenda kuwanufaisha na wao.

Amesema mradi wa reli ya kisasa ni miongoni mwa miradi mikubwa inayotekelezwa kwa ufanisi na Serikali ya CCM chini ya uongozi wa Rais Samia.

Ahadi nyingine ni uchimbaji wa mabwawa na ujenzi wa skimu za umwagiliaji ambapo katika majimbo hayo amesema miradi hiyo itachagiza ukuaji wa sekta ya Kilimo katika maeneo hayo na Tanzania kwa ujumla.

“Ndugu zangu wana Tabora, watani zangu kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wetu na ndio maana mnaona tunafanya kila aina ya njia kuhakikisha kilimo kinaimarika ili kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja,” amesema Dk Nchimbi ambaye yeye ni Mngoni.


Amesema mradi huo unapita katika Wilaya za Uyui na Jimbo la Igalula kwa vipande vifuatavyo: Makutopora–Tabora (km 368), Tabora–Isaka (km 165), Mwanza–Isaka (km 341), Tabora–Kigoma (km 508) na Uvinza–Musongati (km 282). Tutahakikisha unakamilika kwa ubora na muda uliopangwa,” amesema Dk Nchimbi.

Amesema pamoja na mafanikio hayo, Serikali imeendelea kuimarisha usalama na amani ya nchi, jambo lililowezekana kutokana na uwekezaji mkubwa katika vyombo vya ulinzi na usalama.

“Katika kipindi cha miaka minne na nusu ya Mama Samia, Serikali imesimamia usalama na amani ya nchi yetu. Imeimarisha vyombo vya ulinzi na usalama kupitia mafunzo, ajira mpya, vitendea kazi na mbinu za kivita. Leo, majeshi yetu ni imara kuliko wakati mwingine wowote,” amesema.

Katika sekta ya kilimo, Dk Nchimbi amesema Serikali ya CCM itaendeleza mapinduzi ya kilimo kwa kuwezesha wakulima kupata vifaa vya kisasa, maofisa ugani wa kutosha na mafunzo ya kitaalamu ili kuongeza uzalishaji.

Aidha, amebainisha kutajengwa bwawa jipya litakalosaidia miradi ya umwagiliaji na kuongeza tija kwa wakulima wa Igalula.

Kuhusu biashara, Dk Nchimbi amesema kutajengwa masoko ya kisasa katika majimbo hayo na kuboresha mazingira ya biashara hasa kwa kutoa mikopo ya asilimia kumi kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

“Mikopo hii tunakwenda kuiongeza ili kutoa mikopo mikubwa zaidi kwani wajasiriamali au wafanyabiashara ndogondogo wanakuwa pia hawawezi kuwa hao hao kila siku,” amesema.

Pamoja na mambo mengi ambayo chama hicho kinakusudia kuyafanya kwa wananchi ikiwa ni utekelezaji wa ilani yake kimesema kitahakikisha majosho yanajengwa na kuboresha yale yaliyopo na kutoa chanjo ya ruzuku ya mifugo, ili kuepusha magonjwa kwa mifugo hiyo.

Aidha mgombea ubunge wa Igalula, Juma Kawamba amemuomba Dk Nchimbi endapo CCM itaingia madarakani iboreshe miundombinu ya barabara katika jimbo hilo kwani kwa sasa hazipitiki majira yote.

Kwa upande wake, mkazi wa Tabora, Himidi Tweve amesema amani ni jambo muhimu zaidi ya yote huku akiisisitiza CCM ikiingia madarakani kuimarisha zaidi sekta ya kilimo kama ilivyoahidi pamoja na kujenga kwa haraka viwanda hivyo vya tumbaku na mbolea.

“Viwanda tunahitaji sana kwani sisi ni wakulima na si hivyo tu bali mbolea ikitokea Tabora hapa hapa ni nzuri zaidi tunaamini hata bei itapungua,” amesema.

Rhoda Kulwa amesema ahadi iliyotolewa na chama hicho hasa ya kuongeza mikopo ya asilimia kumi itawasaidia kukuza zaidi biashara zao.




“Sasa hivi wanawake tumeamka sana sio tegemezi kama zamani kwa hiyo CCM ihakikishe inatimiza hizi ahadi ambazo kimsingi ni faida kwetu,” amesema.