Dodoma. Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imetangaza huduma yake mpya ya upatikanaji wa vibali, leseni na utatuzi wa malalamiko kupitia mifumo ya kidijitali.
Hatua hiyo imetajwa kuwa itawawezesha wananchi kupata huduma popote walipo na kwa wakati bila kulazimika kufika ofisini ambapo baadhi walilazimika kusafiri umbali mrefu.
Hayo yamebainishwa leo Jumatatu Oktoba 7, 2025 na Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Dk James Andilile wakati akizindua maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja, katika ofisi za Ewura makao makuu, Dodoma.
Dk Andilile amesema huduma hizo zilishaanza kutolewa na kwamba hayo ni mageuzi makubwa katika mifumo ya kiutendaji kazi.
“Tumeendelea kuboresha mifumo ya kidijiti ambayo imeimarisha utoaji wa huduma kwa kasi zaidi na kwa wakati na kuondoa malalamiko ya ucheleweshwaji yaliyokuwepo awali,” amesema Dk Andilile.
Amesema Ewura inatumia mifumo kadhaa ya kidijiti ikiwamo E- LUC, ambao unasaidia kupokea mrejesho na maoni ya wateja juu ya namna wanavyopokea huduma zinazodhibitiwa kutoka kwa watoa huduma wanaosimamiwa na Ewura.
Boniface Malanja amesema kwa sasa wanatumia simu kupata huduma za maombi ya leseni na vibali vinginevyo, jambo ambalo halikuwepo awali.
Malanja amesema teknolojia zinasaidia kurahisisha mambo lakini akasisitiza mifumo kuwa imara wakati wote ili watu wengi wakimbilie huko badala ya kutunga foleni kusaka huduma.
Mfumo unaosifiwa ni wa LOIS unaorahisisha maombi ya leseni, vibali vya ujenzi wa miundombinu ya bidhaa zinazodhibitiwa na uwasilishaji wa malalamiko yanayohusu huduma za nishati na maji.