JKT Queens kujichimbia Uturuki kujiandaa CAFWCL

JKT Queens imepanga kuondoka Tanzania Oktoba 9, 2025 kuelekea Uturuki itakapoweka kambi ya wiki mbili kujiandaa na mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake yatakayofanyika nchini Algeria Novemba 2025.

Akizungumza na Waandishi wa Habari, Ofisa Habari wa JKT Queens, Masau Bwire amesema malengo ya kuweka kambi Uturuki ni kutokana na hali ya hewa ya jiji la Istanbul kuendana na Algeria yanakofanyika mashindano hayo.

“Kwa sasa timu iko kambini na tunatarajia kwenda Uturuki kwa ajili ya maandalizi ya mashindano hayo yatakayofanyika Algeria, tutakuwa mji wa Istanbul tukiutumia Uwanja wa Sancaktepe, tukiwa huko tutacheza mechi mbili za kirafiki na timu zinazoshiriki Ligi ya Wanawake,” amesema Bwire na kuongeza.

“Tumeyapa uzito wa hali ya juu mashindano haya, msimu wa kwanza hatukufanya vizuri na hiyo hali hatutaki ijirudie tena msimu huu lengo ni kufanya vizuri na kuleta heshima kimataifa na Cecafa kwa ujumla.”


Akitolea ufafanuzi juu ya ushiriki wa JKT Queens kwenye mashindano ya Ngao ya Jamii yanayotarajiwa kuchezwa Oktoba 9, 2025 na timu hiyo imepangwa kuumana na Yanga Princess Bwire amesema: “Sisi JKT tuna timu nyingi za vijana na kwa ubora wao tunaamini wataenda kupeleka kichapo cha Kizalendo na watafanya vizuri, kwa sababu wamekuwa na timu kwa muda mrefu.”

JKT Queens ambayo ni bingwa wa Cecafa, inaungana na timu saba kutoka kanda tofauti kukipiga ili kutafuta bingwa wa Afrika kwa wanawake taji linalotetewa na TP Mazembe ya DR Congo.

Timu zitakazoshiriki ambazo ni mabingwa wa kanda ni TP Mazembe ikiwa ni bingwa mtetezi, Gaborone United (Botswana-COSAFA), USF AS Bamako (Mali-WAFU A), ASEC Mimosas ( Ivory Coast-WAFU B), 15 De Agosto Femenino ( Equatorial Guinea-Uniffac) na AS FAR (Morocco-UNAF).

Hii ni mara ya pili kwa JKT Queens kiushiriki mashindano hayo, mara ya kwanza ilicheza mwaka 2023 nchini Ivory Coast na haikufanya vizuri, ikaishia hatua ya makundi.

JKT Queens ndio timu pekee itakayocheza mashindano hayo mara nyingi kwa ukanda wa CECAFA tangu Ligi ya Mabingwa ianzishwe mwaka 2021, timu nyingine zilizowahi kushiriki mashindano hayo ni Vihiga Queens ya Kenya mwaka 2021, Simba Queens Tanzania (2022) na CBE (Ethiopia 2024).

Kwa ukanda huo Simba pekee ndiye ilifika hadi nusu fainali na kufungwa bao 1-0 na Mamelodi Sundown ya Afrika Kusini ikamaliza nafasi ya nne.