Kaka, dada jela kwa kosa la kuoana

Maswa. Mahakama ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, imewahukumu kifungo cha miaka 20 na 30 jela ndugu wa damu baada ya kupatikana na hatia ya kosa la kuzini na maharimu na kufanikiwa kupata mtoto.

Hukumu hiyo ilisomwa Oktoba 6, 2025 mbele ya Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Maswa, Aziz Khamis katika kesi ya jinai iliyowahusisha Mussa Shija (33) aliyehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela huku dada yake Hollo Shija (36), akihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela, wote wakazi wa Kijiji cha Mandang’ombe wilayani Maswa.

Awali, washtakiwa hao walikuwa wamekiri kosa na kuhukumiwa kifungo cha miaka 20 na 30 jela Agosti 14,2024  lakini walikata rufaa Mahakama Kuu ambayo iliagiza kesi hiyo kusikilizwa upya katika Mahakama iliyowahukumu.

 Wakati wa usikilizwaji upya Mei 6,2025 walisomewa mashtaka yao ambayo ni Kuzini na Mahrimu kinyume na kifungu cha 158(1)(b)na 160cha Sheria ya kanuni ya adhabu sura 16 Marejeo ya mwaka 2022 , walikana shtaka hilo wakidai kuwa ni wanandoa halali waliolipiana mahari na mlalamikaji alisababisha kesi hiyo kutokana na chuki binafsi.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Khamis amesema kitendo cha washtakiwa kimevunja misingi ya kimaadili na kisheria, na pia kinakwenda kinyume na maadili ya jamii, kwa kuwa ni kosa la wazi la zinaa na maharimu.

“Ni wajibu wa mahakama kulinda maadili ya jamii na sheria za nchi. Hawa ni ndugu wa damu waliogeuza uhusiano wao wa kifamilia kuwa wa kindoa, jambo ambalo si la kukubalika kisheria wala kimaadili,” amesema.

Kwa mujibu wa mashtaka yaliyowasilishwa na upande wa Jamhuri ukiongozwa na Mkaguzi wa Polisi, Vedastus Wajanga, washtakiwa waliishi kama mume na mke kuanzia mwaka 2018 hadi Julai 2024 na kupata mtoto mmoja wa kiume.

Kwa upande wa mashtaka uliwasilisha  mashahidi 11 na vielelezo vitano, ikiwemo ripoti ya uchunguzi wa vinasaba (DNA) kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali iliyoonesha kwa asilimia 99.99 Musa na Hollo ni watoto halali wa baba mmoja, Shija Kamuga, na mtoto waliyezaliwa naye pia ni wa damu yao.

Mahakama baada ya kuwakuta na hatia iliwapatia nafasi ya kujitetea ambapo mshtakiwa wa kwanza Mussa Shija alidai kuwa yeye ni yatima wazazi wake walifariki na kumuacha akiwa mtoto mdogo na kulelewa na bibi yake mzaa mama, na Hollo Shija ni mke wake halali ambaye amemtolea mahali ya Sh325,000 na alimpa bibi yake na Hollo, mzaa mama.

Naye Mshtakiwa wa pili, Hollo Shija alidai kuwa na yeye ni yatima wazazi wake walifariki akiwa mdogo na amelelewa na bibi yake mzaa mama na Mussa Shija ni mume wake halali wa ndoa.

Pia, wote walidai kuwa Shija Kamuga ni jirani yao tu na hii kesi kawasingizia tu kwa sababu ana wivu na chuki na ndoa  yao, na sio baba yao mzazi.

Upande wa mashtaka uliomba washtakiwa wapewe adhabu kali ili iwe fundisho kwao na onyo kwa wengine wenye nia au lengo la kufanya kitendo walichokifanya, ukizingatia kuwa kitendo cha kujamiiana na ndugu wa damu ambaye ni kaka na dada na kuishi kama mke na mume pamoja kuzaa mtoto, ni cha ajabu na cha aibu na kinyume cha maadili ya Kitanzania na ya Mwafrika kwa ujumla.