Kocha JKT aitoa tuzo kwa wachezaji

BODI ya Ligi imemtangaza Ahmad Ally wa JKT Tanzania kuwa kocha bora wa Ligi Kuu Bara mwezi uliopita, lakini kocha huyo ameitoa tuzo hiyo kwa wachezaji wa kikosi hicho akisema ndio waliovuja jasho.

Ahmad amesema tuzo hiyo inayomfanya kuwa kocha wa kwanza kuibeba kwa msimu wa 2025-2026 imetokana na wachezaji wa kikosi hicho kuvuja jasho jingi uwanjani wakiipambania timu ili kupata matokeo ya ushindi.

Kocha huyo aliyewashinda Romain Folz wa Yanga na Miguel Gamondi wa Singida Black Stars, alipata tuzo hiyo baada ya timu ugenini kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Mashujaa, ikashinda mabao 2-1 dhidi ya Coastal Union na kutoka sare ya 1-1 na Azam FC ikiwa katika uwanja wa nyumbani.

JK 03


“Japo tuzo hiyo nimeipata mimi, lakini ni maalumu kwa ajili ya wachezaji ambao wanajituma uwanjani na kuzingatia mbinu ninazowapa pia na stafu ninaofanya nao kazi,” amesema Ahmad na kuongeza:

“Imetupa morali ya kuendelea kupambana kwa sababu Ligi Kuu ya msimu huu ndiyo imeanza bado safari ni ndefu, inayohitaji kujituma zaidi.”

Alipoulizwa tetesi za kuhusishwa na Simba zina ukweli gani, kocha huyo alijibu: “Siwezi kuzungumzia timu nyingine wakati nina mkataba na JKT Tanzania na kama watahitaji huduma yangu, basi wawatafuata waajiri wangu wazungumze nao.”

JK 02


Mbali na hilo amewataja makocha ambao alikuwa anaendana nao kimbinu na alikuwa anajifunza vitu vingi kutoka kwa Fadlu Davids aliyeachana na Simba na Youssouph Dabo aliyewahi kuinoa Azam.

“Aina ya wachezaji waliokuwa wanawatumia na mbinu zao tunaendana, hivyo kuna baadhi ya vitu nilikuwa najifunza kutoka kwao, siyo kwa sababu ya ugeni wao hapana,” amesema kocha huyo.