Lissu aibua mapya, kesi yake ya uhaini

Dar es Salaam.  Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, anayekabiliwa na kesi ya uhaini, ameibua mambo mapya mahakamani akidai kuwa kesi hiyo imepangiwa tarehe ya hukumu kabla haijaanza kusikilizwa.

Lissu amedai kuwa kwa mujibu wa taarifa za maandishi alizopelekewa gerezani kutoka kwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, Livin Lyakinana, kesi hiyo imepangwa kutolewa hukumu Novemba 12, 2025.

Lissu ameibua madai hayo leo Jumatatu, Oktoba 6, 2025 kabla ya kuanza usikilizwaji wa kesi hiyo.

Kesi hiyo inayosikilizwa na jopo la majaji watatu, wakiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Iringa, Dunstan Ndunguru, akishirikiana na majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde, imepangwa kuanza kusikilizwa ushahidi wa Jamhuri leo.

Alipoitwa baada ya utambulisho wa pande zote, kabla ya kesi kuanza, Lissu ameiomba Mahakama kuwa kabla ya kuanza kusikiliza ushahidi huo, ana mambo matatu na anataka Mahakama imsikilize.


Lissu ameanza kwa kusema kuwa Agosti 30, 2025, Naibu Msajili Livin Lyakinana alimwandikia barua kupitia Mkuu wa Gereza ambayo alikabidhiwa Oktoba 2, 2025.

Amedai kuwa barua hiyo ilimwelekeza kuwa awasilishe orodha ya watu 100 ambao angependelea wahudhurie kesi hii na kwamba majina hayo yamfikie Naibu Msajili Oktoba 3, 2025 kabla ya saa 12 jioni na watu hao ni pamoja na mawakili, viongozi wa chama na ndugu zake.

Amedai kuwa kwa kuwa yuko gerezani ambako hana mawasiliano na ndugu zake, mawakili na hata viongozi wa chama, lakini pamoja na ugumu huo alihangaika akiwa peke yake akafanikiwa kuandika majina hayo 100 na akayawasilisha Ijumaa kabla ya saa 12 kama alivyoelekezwa.

Hata hivyo, amedai kuwa, leo, kati ya watu aliowaandika, ndugu yake amezuiliwa kuingia na amemuona mwenyewe huku jina lake ni la 12, Dk Stephan Lincoln ambaye ametoka Ujerumani kwa ajili ya kusikiliza kesi hiyo, pamoja na Almquist Knopf kutoka Marekani.

Lissu amedai kuwa licha ya hao waliozuiliwa, pia amedai kuna watu wamepigwa nje, akisema kuwa   anataka kujua kama hiyo Mahakama ni ya Polisi na nani anayehusika kuwazuia watu.

Amehoji kulikuwa na maana gani kuambiwa alete majina halafu watu hao wanazuiliwa.


“Hili waheshimiwa majaji si la kiutawala, hili ni la kisheria, ni suala la Kikatiba. Mahakama hii ni Mahakama Kuu kweli ya Tanzania au ni jina tu na wanaoamua mambo yaendeje ni mapolisi,” amesema na kuongeza:

“Kwa hiyo naomba hao waliozuiliwa waruhusiwe kuingia na hao waliopigwa waruhusiwe kuingia ili tuweze kuendelea.”

Jambo la pili, Lissu amedai kuwa Oktoba Mosi, 2025 aliandikiwa barua tena na Naibu Msajili hiyo, Lyakinana iliyomfikia Ijumaa Oktoba 3, 2025 mchana ikimjulisha kuhusu kikao cha awali kabla ya usikilizwaji kesi (pre-session meeting) ambacho kilipangwa kufanyika siku hiyo saa 8 mchana kwa mtandao.

Amedai kuwa alimwambia ofisa wa magereza aliyekabidhiwa barua hiyo awaeleze walioipeleka wampelekee taarifa sahihi na si taarifa ya saa mbili na hivyo hakuhudhuria kikao hicho kwa sababu hiyo.

Lissu amehoji na kuomba Mahakama imueleze hicho ni kitu gani katika sheria za Tanzania.

Lissu amesema kikao hicho kwenye kesi za jinai ni hakipo katika sheria anazozifahamu.

Pia, amedai kuwa katika barua hiyo kuna kiambatanisho ambacho (cause list – ratiba ya vikao vya mashauri) kinaeleza kuwa kesi hiyo itasikilizwa kuanzia leo Oktoba 6, 2025 mpaka 24 na  baada ya hapo kutakuwa na mapumziko ya siku 10 ambapo itaendelea tena kuanzia Novemba 3 mpaka 12, 2025.

Lissu amedai kuwa hicho kiambatanisho ndicho kilichomstua.

Amebainisha kuwa ingawa hati ya wito inasema kesi itasikilizwa mpaka Oktoba 24, 2025 lakini kiambatanisho hicho  kinaonesha kuwa inakwenda mpaka Novemba 12, 2025 na ndiyo siku ya hukumu.

Lissu amehoji kuwa inakuwaje kesi ina mashahidi 30 wa Jamhuri na wa kwake 15 na haijaanza kusikiliza hata shahidi mmoja lakini imeshapangwa mpaka tarehe ya hukumu, huku akihoji kama tayari majaji wameshaandika hukumu hata kabla ya kesi kusikiliza.


“Kama tayari mnayo hukumu basi nihukumuni tu,” amesema Lissu.

Amehoji kuwa nani anaandika mambo kama hayo na kwa mamlaka gani huku akisisitiza kuwa anaomba majibu katika hayo kabla ya kuendelea.

Kutokana na madai hayo Mahakama imeahirishwa kwa nusu saa kabla ya kuja kutoa ufafanuzi wa hoja hizo za Lissu.

Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyoyatamka kuhusiana na kuzuia kufanyika uchaguzi mkuu wa baadaye mwaka huu.

Anadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania, kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyika kwa uchaguzi mkuu, kwa lengo la kuitishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuchapisha maneno yafuatayo:-

“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kukinukisha…sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”

Lissu alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Aprili 10, 2025 na kusomewa shtaka hilo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, Kisutu, alikofikishwa kwa ajili ya maandalizi ya awali ikiwemo kukamilisha upelelezi kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu, kwa ajili ya usikilizwaji kamili.

Baada ya upelelezi kukamilika kesi hiyo ilihamishiwa  Mahakama Kuu Agosti 18, 2025 kwa ajili ya usikilizwaji kamili.